Rais wa FIFA, Sepp Blatter |
Rais wa TFF, Leodeger Tenga |
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam leo, Rais wa TFF, Leodeger Tenga, amesema kuwa sasa uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 24, hautafanyika tena na hatma yake itategemea ripoti ya tume ya FIFA itakayotua nchini katikati ya mwezi ujao.
Uchaguzi huo ulikuwa umeambatana na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wadau wa soka nchini baada ya TFF kupitia kamati yake ya Rufani kuwaengua wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi aliyekuwa akiwania nafasi ya urais na Michael Wambura aliyetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.
Kutokana na uamuzi wa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake Iddi Mtiginjola, nafasi ya urais ilibakiwa na mgombea mmoja tu, Athumani Nyamlani, ambaye hivi sasa ndiye Makamu wa Rais wa TFF.
Katika hatua nyingine, Tenga amesema kuwa ushauri alioutoa hivi karibuni kwa kina Malinzi, Wambura na wengine wanaopinga kuenguliwa kwa kuwataka wafuate njia tatu ulitokana na mawazo yake binafsi na wala si vinginevyo.
Tenga alikaririwa akiwaasa kina Malinzi kuwa wanaweza kufuata njia tatu, ambazo ni kwenda kushitaki FIFA, kupeleka shauri hilo kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) au kuomba kamati ya kina Mtiginjola ipitie upya maamuzi yake; mapendekezo ambayo kina Malinzi waliyatekeleza kwa kuomba kamati ya rufani ipitie upya maamuzi hayo.
Hata hivyo, Mtiginjola alipinga pendekezo la Tenga la kutaka kupitiwa upya kwa maamuzi yaliyowaondoa kina Malinzi kwa kusema wazi kwamba kanuni hazielekezi hivyo na badala yake akawataka wasioridhika na maamuzi ya kamati yake waende kushitaki CAS.
TAARIFA KAMILI YA TFF:
FIFA YASITISHA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF
SHIRIKISHO la Kimaifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeahirisha uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mkanganyiko uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam leo mchana (Februari 19 mwaka huu), Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema FIFA imetuma barua ikiagiza mchakato wa uchaguzi usimame baada ya kupata malalamiko.
Amesema kutokana na mkanganyiko huo, FIFA katika barua yake ya leo (Februari 19 mwaka huu- imeambatanishwa) imeagiza mkutano wa uchaguzi wa TFF ambao awali ulipangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu uahirishwe hadi hapo itakapotuma ujumbe wake nchini.
Ujumbe huo wa FIFA unatarajiwa kufika nchini katikati ya mwezi ujao (Machi) ambapo utafanya tathimini ya hali hivyo, kutuma ripoti yake katika shirikisho hilo na baadaye kutoa mwongozo wa nini kifanyike.
Rais Tenga amewaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na uamuzi huo wa FIFA, hivyo kwa sasa hakutakuwa tena na mkutano huo mpaka hapo watakapopewa taarifa nyingi.
Amesema TFF inakaribisha kwa mikono miwili uamuzi huo wa FIFA kwa sababu ni chombo ambacho cha juu kimpira duniani, na hatua hiyo ina lengo la kuhakikisha kuwa kila mhusika katika mchakato huo wa uchaguzi anapata haki yake.
“Nia yetu ni kuona watu wanatendewa haki, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli. Hivyo wahusika (waathirika) wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja zao ili FIFA wakifika wawasikilize, wapate maelezo ya kina kuhusu utaratibu na malalamiko yaliyotolewa,” alisema Tenga.
Rais Tenga amesema timu hiyo ya FIFA itakapofika yenyewe ndiyo itakayopanga izungumze na nani kwa wakati gani, hivyo ni vizuri waathirika na vyombo vyote vilivyohusika na mchakato wa uchaguzi wakajiandaa.
Amesema ilikuwa ni muhimu suala hili likatatuliwa katika ngazi ya FIFA kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi utakapofanyika TFF inaendelea kuwa chombo kimoja badala ya kurudi katika migogoro iliyokuwepo huko nyuma.
“Nataka tubakie kama tulivyokuwa. Malumbano yaishe. Pangeni hoja, wakija hao waheshimiwa (FIFA) muwaambie. FIFA ni chombo cha juu, nafurahi wamekubali kuingia katika hili, kwani wana shughuli nyingi wangeweza kukataa,” amesema.
Kuhusu fursa ya kufanya marejeo (review) kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inayoongozwa na Idd Mtiginjola ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga amesema kwa vile hicho ndicho chombo cha mwisho nchini katika masuala ya uchaguzi alishauriwa kuwa kingeweza kufanya review.
“Kwa vile hakuna chombo kingine, nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya review. Katika utaratibu wa kutoa haki, uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa sababu. Nilidhani hilo linawezekana, kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo. Kwa hili uamuzi wa Mtiginjola ni sahihi,” amesema Rais Tenga.
Kamati ya Mtiginjola iliyokutana jana (Februari 18 mwaka huu) ilitupa maombi ya review yaliyowasilishwa mbele yake na waombaji uongozi watano kwa vile hakuna kipengele chochote kwenye Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi kinachotoa fursa hiyo.
Waombaji hao walikuwa Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wengine ni walioomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano; Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).
No comments:
Post a Comment