Wednesday, February 20, 2013
SIMBA YANGURUMA MBEYA... AZAM YAIFIKIA YANGA
MNYAMA Simba aliweka kando matokeo mabaya katika siku za karibuni na kuilaza Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya, huku Azam wakiendelea kutoa onyo kali kwa wapinzani wao wa Jumamosi Yanga kwa kuichakaza JKT Ruvu kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi leo.
Amri Kiemba alifungia bao pekee lililoamua mechi mjini Mbeya kufuatia pasi tamu ya Haruna Moshi 'Boban' na kuifanya Simba ijiimarishe katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kufikisha pointi 31 kutokana na mechi 17.
Ushindi wa Azam unamaanisha kwamba wameifikia Yanga juu ya msimamo kutokana na kuwa na pointi 36, lakini timu ya Jangwani inaendelea kubaki kileleni kutokana na tofauti nzuri ya mabao.
Khamis Mcha alifunga magoli mawili, John Bocco moja na Abdi Kassim 'Babi' moja wakati Azam walipotoa kipigo kikubwa cha pili mfululizo katika ligi baada ya kushinda 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini Manungu katika mechi yao iliyopita. Baada ya mechi hiyo, Azam waliifunga Al Nasri ya Sudani Kusini kwa magoli 3-1 katika mechi yao ya Kombe la Shrikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
Coastal Union ya Tanga nayo imejiimarisha katika nafasi ya nne kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na hivyo kufikisha pointi 30 baada ya mechi 18.
Toto African iliondoka kwenye ukanda wa kushuka daraja kwa kupanda nafasi moja juu hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo baada ya kushinda 2-0 dhidi ya timu inayoburuta mkia ya African Lyon yenye pointi 9. Toto sasa imefikisha pointi 17, moja nyuma ya Prisons iliyo katika nafasi ya 10.
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment