Wednesday, February 6, 2013

MOURINHO AKERWA WACHEZAJI REAL MADRID KUIPOTEZEA LA LIGA NA KUIKAMIA MECHI YA LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA DHIDI YA MAN U…!


José Mourinho aliona ni kitu gani kingetokea kwa timu yake ya Real Madrid kabla ya mechi yao ya ugenini dhidi ya Granada. Na hicho ndicho kilichomfanya atumie dakika kadhaa kwenye vyumba vya kuvalia kabla ya kuchezwa kwa mechi hiyo waliyolala 1-0, akiwakumbusha wachezaji wake kuwa kadri wanavyocheza vizuri katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania ndivyto wanavyojiwekea mazingira mazuri ya kufanya vyema katika mechi yao ijayo ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Manchester United na pia ya marudiano kwenye Kombe la Mfalme dhidi ya Barçelona.

"Mnapaswa kuzingatia fahari ya weledi wenu kwa kucheza katika kiwango chenu cha juu katika kila mechi. Mnapaswa kujituma sana na siyo kubweteka, tena katika kila michuano."
Huo ndiyo ujumbe alioutoa Mourinho kwa wachezaji wake bila kupindisha maneno, muda mfupi kabla ya mechi yao dhidi ya Granada.

"Kuwa wa pili ni bora kuliko kushika nafasi ya tatu, na kuwa nyuma ya Barca kwa pointi tano au sita ni bora kuliko kuachwa kwa pointi 15 au 16", ulikuwa ni ujumbe mwingine wa kocha huyo Mreno kwa wachezaji wake.

Kwahiyo, kuhuzunika kwa Mreno huyo kufuatia kichapo walichopata kutoka kwa Granada kilitokana zaidi na namna timu ilivyocheza na siyo matokeo.

"Matokeo hayakunisumbua sana, lakini kiwango cha timu katika kipindi cha kwanza hakikunifurahisha kabisa; kilikuwa cha hovyo. Tulitawala katika kipindi cha pili na kupata nafasi chache za kufunga na kusawazisha, lakini hilo peke yake halikutosha kunipa furaha," alisema Mourinho.

Real Madrid watashuka dimbani Jumatano ijayo kucheza nyumbani mechi yao ya kwanza ya hatua ya 16-bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Man U na Februari 27 watarudiana na Barcelona katika mechi yao ya ugenini ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme kwenye Uwanja wa Camp Nou. Katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Barca, matokeo yalikuwa sare ya 1-1.

No comments:

Post a Comment