Sunday, February 10, 2013

MALI WASHINDI WA TATU TENA... YAIZAMISHA GHANA 3-1

Mahamadou Samassa akishangilia bada ya kuifungia Mali goli la kwanza
Ghana wakishangilia goli lao

MALI walimaliza wakiwa washindi wa tatu wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2013 baada ya kuibwaga Ghana iliyopoteza matumaini kwa magoli 3-1.

Matokeo hayo ni marudio ya ushindi wa Mali dhidi ya Ghana, kwani katika fainali za mwaka jana nchini Gabon timu hizo pia zilikutana katika kutafuta mshindi wa tatu na Mali ikashinda 2-0.

Baada ya kupoteza nafasi ya kutwaa kombe hilo, Ghana na Mali sasa zinaweka nguvu zake katika kusaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.

Mahamadou Samassa aliipatia Mali goli la kuongoza katika dakika ya 21 ambalo lilidumu hadi wakati wa mapumziko.

Mali walianza vyema kipindi cha pili kwa kuongeza goli la pili lililofungwa na nahodha wao nyota wa zamani wa klabu ya Barcelona, Seydou Keita, katika dakika ya 48.

Ghana walipata goli moja lililofungwa kwa shuti la mbali na Kwadwo Asamoah katika dakika ya 81 lakini wakati wakijaribu kuongeza presha langoni mwa Mali ili kulazimisha mechi iende kwenye hatua ya matuta, walijikuta wakifungwa goli la tatu na mtokea benchi
Sigamary Diarra katika za majeruhi.

Nigeria na Burkina Faso zitachuana leo katika kusaka bingwa wa fainali za Mataifa ya Afrika 2013.

No comments:

Post a Comment