Sunday, February 10, 2013

BOLT, BLAKE WAANZA MSIMU KWA KUSHIRIKI MITA 400 JAMAICA

Bolt (katikati) akiwa na Blake (kushoto) na Weir (kulia)

MABINGWA wa Olimpiki, Usain Bolt na Yohan Blake walifungua msimu wao wa 2013 kwa kushiriki mbio za mita 400 nchini kwao Jamaica.

Wote wawili walikuwa wakiiwakilisha klabu yao ya Racers Track katika mashindano ya Camperdown Classic kwenye Uwanja wa Taifa mjini Kingston.

Bolt alimpita Allodin Fothergill katika kumalizia na kushinda mashindano hayo ya mchujo akitumia muda wa sekunde 46.74 - muda ambao ni mbali kabisa ya muda wa rekodi ya dunia uliowekwa na Michael Johnson wa sekunde 43.18.

Blake alikuwa wa pili katika kundi lake la mchujo ambapo alitumia muda wa sekunde 46.64, nyuma ya patna wake wa mazoezi Warren Weir. Bolt, Blake na Weir wanafanya mazoezi pamoja.

Weir ndiye aliyekimbia kwa kasi zaidi katika mbio hizo za mchujo za jana usiku baada ya kutumia sekunde 46.23.

Hapakuwa na mbio za fainali katimka mchujo huo ulioshirikisha wanariadha 30.

"Nilijisikia hofu kiasi," alisema Bolt, ambaye anashikilia rekodi ya duniani ya mita 100 na mita 200.

"Nilikuja hapa kushinda na nina furaha nimeshinda bila ya kupata majeraha."

Blake alisema: "Nimefurahia mbio hizo, licha ya muda nilioutumia. Naangalia mbele kwa ajili ya msimu mzima."

No comments:

Post a Comment