Wednesday, February 6, 2013

LIONEL MESSI AIKATALIA BARCELONA KUONGEZA DAU LA KUVUNJA MKATABA WAKE... ASAINI MKATABA MPYA UNAOMBAKISHA HADI 2018 LAKINI MIHELA YA KUMNG'OA BARCA ILI AENDE KOKOTE YABAKI KUWA SH. BILIONI 535

Leo Alhamisi (Februari 6, 2013), Leo Messi amesaini mkataba mpya wa kuichezea Barcelona, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo chini ya utawala wa rais wa sasa wa klabu hiyo, Sandro Rosell.

Moja kati ya mambo yaliyozua mabishano makali wakati wa mazungumzo kabla ya kufikia makubaliano ya mkataba huo mpya ni kipengele cha kuuvunja pindi mwanasoka huyo bora wa dunia akitaka kuondoka kabla ya kumalizika kwa mkataba huo. Barcelona walitaka kuongeza gharama za kuvunja mkataba huo kutoka dau la awali la euro milioni 250 (Sh. bilioni 535), lengo likiwa ni kuongeza ugumu kwa klabu yoyote itakayotaka kumtwaa.

Messi, hata hivyo, alisimama imara na kukataa kabisa kuongezwa kwa dau la kumng'oa. Ni kweli, hafikirii kuhamia klabu nyingine kwa sasa. Hata hivyo, huwezi kujua nini kitakachotokea, kadri aonavyo mwenyewe, ingawa euro milioni 250 ni fedha 'kiduchu', na mabilionea wanaomiminika kuwekeza katika klabu za soka wanaweza kushawishika kirahisi kulipa kiasi hicho ili kuvunja mkataba wake. Barça wanalijua hilo, na ndiyo maana kwa kuanzia wakataka kupandisha dau la kuvunjia mkataba wake, lakini Messi hakutaka kabisa kusikia jambo hilo na kuwagomea.

Muargentina huyo alikuwa akitaka kuongezwa mshahara ili kufidia makato ya kodi mpya ya mapato iliyoongezwa na serikali ya Hispania, ambayo ingemfanya afyekwe euro milioni moja (Sh. bilioni 2.14) katika mshahara aliokuwa akilipwa mwaka uliopita. Klabu ilikubaliana na ombi lake kwa kuongeza mshahara wake hadi kufikia euro milioni 12 (Sh. bilioni 26) kwa kila msimu baada ya makato ya kodi hadi mwaka 2018.

Mchawi huyo wa soka atadaka 'mkwanja' mwingine zaidi unaofikia euro milioni 4 (Sh. bilioni 9) kwa mwaka ikiwa ni nyongeza ya posho itokanayo na kiwango atakachokuwa akionyesha. Fedha hizi za motisha ni pamoja na mataji ambayo klabu hiyo itayatwaa, mechi atakazocheza na pia ikiwa atashinda tena kwa mara ya tano Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia (FIFA Ballon d'Or) -- tuzo ambayo hii peke yake itamhakikishia kitita cha euro milioni moja (Sh. bilioni 2.14) kila mwaka atakapoitwaa.

No comments:

Post a Comment