Sunday, February 10, 2013

AZAM WAIKAMATA YANGA BAADA YA KUIKANDAMIZA MTIBWA 4-1

Kipre Tchetche
Straika wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche ameonyesha kiwango cha juu na kufunga magoli mawili wakati akiisaidia Azam kuibuka na ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Manungu uliopo Turiani, Morogoro leo.

Magoli mengine yaliyoihakikishia ushindi  Azam yaliwekwa wavuni na wachezaji wao wengine wa kimataifa,  Mganda Brian Umony na Mkenya Aturdo,  wakati goli la kufutia machozi la Mtibwa likifungwa na winga wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Vicent Barnabas.

Kwa ushindi huo, Azam sasa wameikamta Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ya Bara baada ya kufikisha pointi 33, lakini wakiendelea kukamata nafasi ya pili kwa tofauti ya magoli. Hata hivyo, Yanga wana mechi moja zaidi mkononi ambayo watacheza keshokutwa dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .

Magoli mawili aliyofunga leo yamemfanya Kipre Tchetche afikishe magoli 10 na hivyo kuendelea kutesa kileleni mwa orodha ya wafungaji wanaoongoza katika ligi kuu ya Bara, akimuacha kwa mabao mawili straika wa Yanga, Mrundi Didier anayemfuatia katika nafasi ya pili.

No comments:

Post a Comment