Tuesday, January 29, 2013

ZAMBIA WAVULIWA UBINGWA AFRIKA... NIGERIA YASHINDA "USIKU", SASA KUWAVAA IVORY COAST KWENYE ROBO FAINALI

Victor Moses wa Nigeria akikimbilia mpira wakati wa mechi yao dhidi ya Ethiopia leo, Nigeria walishinda 2-0 magoli yote yakifungwa na Moses kwa penalti.

Tumewavua ubingwa... Wachezaji wa Burkina Faso wakishangilia baada ya sare yao ya 0-0 dhidi ya Zambia iliyowavua ubingwa wa Afrika watetezi hao leo.

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Zambia "Chipolopolo", wamevuliwa ubingwa leo kufuatia sare ya 0-0 dhidi ya Burkina Faso, huku Nigeria wakihitaji magoli mawili ya penalti ya dakika za lala-salama ili kutinga robo fainali kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Ethiopia waliomaliza wakiwa 10 uwanjani.

Nigeria ambao walimaliza wakiwa wa pili nyuma ya Burkina Faso, watawakabili Ivory Coast katika mechi ya robo fainali inayotarajiwa kutazamwa kama fainali.

Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi alisema baada ya mechi hiyo kwamba ushindi wa leo aliusubiri kwa siku nyingi sana na anaamini utawapa faraja Wanigeria kote duniani.

"Kila mechi ina mbinu zake. Tutaingia kuwakabili Ivory Coast kwa mbinu tofauti na tulizotumia kuwakabili Ethiopia leo au hata tulizotumia katika mechi mbili zilizotangulia," alisema mchezaji huyo wa zamani wa Nigeria wakati akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua wanajiandaaje kwa mechi ya ya robo fainali na mbinu gani watakazotumia. "Kuhusu mbinu tutakazotumia siwezi 'kushea' na wewe. Hizo nitashea na wachezaji wangu."

Zambia ambayo ilimuacha nje nahodha wao mhamasishaji, Chris Katongo, aliyewapa ubingwa wao wa kwanza wa Afrika mwaka jana, ilicheza kwa kiwango cha chini huku ikikosa makali katika umaliziaji huku straika wao Collins Mbesuma "akimpasia" kipa wa Nigeria, Vincent Enyeama, kwa kishuti "mtoto" katika nafasi ya wazi zaidi waliyopata Chipolopolo.

Kocha Mfaransa, Herve Renard, aliyewapa ubingwa mwaka jana, alimuacha nje Katongo kutokana na madai ya kucheza chini ya kiwango katika mechi zao mbili za awali, maamuzi ambayo atayajutia.

Burkina Faso iliyocheza kwa kujilinda zaidi ikihitaji sare tu ili kusonga mbele, ilipata pigo la mapema baada ya kinara wa mabao wa fainali hizi, Alain Traore, kuumia katika dakika ya 10 na kutolewa kwa machela. Traore amefunga magoli matatu yakiwamo mawili katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Ethiopia katika mechi yao ya pili.

Zambia pia walipata pigo dakika chache baadaye baada ya nyota wao Davis Nkausu kuumia 'enka' kufuatia kukanyagwa vibaya na nahodha wa Burkina Faso, katika tukio ambalo lilistahili kadi nyekundu lakini halikutoka hata onyo. Nafasi ya Nkausu ilichukuliwa na Joseph Musonda.

Burkina Faso wamemaliza vinara wa kundi hilo kwa kuwa na pointi tano, sawa na Nigeria walio katika nafasi ya pili kutokana na kuzidiwa magoli.

Hii ni mara ya kwanza kwa Burkina Faso kutinga raundi ya pili tangu walipoandaa michuano hiyo mwaka 1998.

Zambia "imefia" katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu baada ya sare tatu. Mabingwa hao walikuwa na maandalizi mabovu kwa kuchapwa mechi tatu, ikiwamo dhidi Tanzania kupitia goli pekee la Mrisho Ngassa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, na sare moja katika mechi zao nne za kujipima kabla ya michuano hiyo.

Mabingwa kutolewa katika hatua ya awali, ni mara ya kwanza tangu mwaka 1992 wakati Algeria walipotolewa katika hatua ya makundi.

Winga wa Chelsea, Victor Moses, ndiye aliyekuwa shujaa wa Nigeria leo baada ya kufunga penalti mbili za dakika za lala salama na kuipeleka timu yake hatua ya robo fainali ambayo kama matokeo yangebaki ya 0-0 ingeaga mashindano.

Moses aliangushwa mara mbili ndani ya boksi na akafunga penalti zote mbili, ya pili langoni akiwa amesimama kiungo, Addis Hintsa, aliyelazimika kuvaa jezi ya kipa baada ya mlinda mlango wa Ethiopia, Sisay Bancha, kutolewa kwa kadi ya pili ya njano huku wakiwa tayari wameshamaliza "sub" zao zote tatu. 

No comments:

Post a Comment