Wednesday, January 2, 2013

VAN MAGOLI: NIMEZUNGUKWA NA MABINGWA MAN UTD

Wachezaji wa Manchester United wakishangilia jana

Pablo Zabaleta (kushoto) akishangilia baada ya kuifungia Man City dhidi ya Stoke City jana.
Dimitar Berbatov (wa tatu kulia) na wenzake wakifurahia ushindi dhidi ya West Brom jana
Gazton Ramirez wa Southampton akishangilia goli la kuongoza alilofunga dhidi ya Arsenal jana.

ROBIN van Persie anaona kwamba "amezungukwa na mabingwa" klabuni Manchester United wakati akielezea namna anavyoamini kwamba watatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 alifunga mara mbili wakati Man U ilipoisambaratisha Wigan 4-0 kwenye uwanja wao wa DW jana.


Ilikuwa ni goli la 19 la Van Persie tangu alipojiunga akitokea Arsenal katika kipindi kilichopita cha usajili.
"Tunapaswa kuangalia hali mechi hadi mechi lakini kila mtu anataka kuwa bingwa. Najiona nimezungukwa na mabingwa," aliiambia MUTV kufuatia ushindi dhidi ya Wigan.


Pointi tatu ziliihakikishia timu ya Sir Alex Ferguson kudumisha tofauti ya pointi saba kileleni juu ya mahasimu wao wa jadi na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City.


Van Persie alibainisha njaa iliyopo ndani ya kikosi cha Man U ya kutaka kurejesha taji lao walilolipoteza kwa Man City kwa tofauti ya pointi msimu uliopita, jambo lililotokea kabla ya yeye kujiunga nao kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 24 Agosti mwaka jana.


"Hii ni timu 'spesho'," aliiambia MUTV. "Kila mtu anataka kumsaidia mwenzake. Kila mtu anataka mwenzake afunge. Mabeki wanafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya viungo wao, viungo wanapambana kwa ajili ya washambuliaji... kila mtu anataka kukimbia na kila mmoja ana lengo moja akilini mwao.
"Wanajua kushinda na hilo linanipa wepesi mimi."


Kocha wa Man U, Ferguson amekiri kwamba alifahamu kuwa Van Persie angeleta mabadiliko makubwa.
Ijumaa, kocha wa Man City, Roberto Mancini alibainisha hofu yake kwamba kushindwa kumnunua Van Persie huenda kukaigharimu kombe timu hiyo.


Van Persie alitia mchango mkubwa tena katika ushindi wa Man U juzi na kuchochea imani ya makocha wote kwamba nyota huyo ndiye atakayeamua bingwa hasa kwa goli lake la kwanza ambalo alimgeuza beki wa Wigan, Ivan Ramis kabla ya kufunga kwenye kona ya juu ya lango akitumia mguu wake "dhaifu" wa kulia.


"Tulijua tunapata mchezaji ambaye wa kiwango cha juu ambaye ataleta tofauti kwenye timu," alisema Ferguson. "Ndio maana tukamfuata.


"Robin ni mchezaji aliyekamilika. Ana uzoefu wa kimataifa, amechezea Arsenal kwa miaka saba na amekuja kwetu akiwa katika kiwango cha juu kabisa cha maisha yake ya soka.


"Uwezo wake wa kupika na kufunga magoli ni bab'kubwa. Alichokifanya wakati akifunga goli la kwanza ilikuwa ni bab'kubwa, alivyogeuka, alivyojibalansi bila ya kuyumba na kuutumbukiza mpira wavuni. Lilikuwa goli zuri sana."


Wakati Van Persie ndiye kinara wa mabao wa Man U, amesisitiza kwamba asingeweza kupata mafanikio hayo mwanzoni mwa maisha mapya Old Trafford bila ya msaada wa wachezaji wenzake.


"Kila mtu anataka kumsaidia mwenzake na kila mtu anataka kushiriki katika kupatikana kwa goli," Van Persie aliongeza.


"Angalia goli la mwisho (dhidi ya Wigan) - Danny alitaka kunipa mpira mimi ili nifunge. Kila mtu yuko hivyo.
"Nami niko hivyo, Chicha (Javier Hernandez) yuko hivyo... kila mtu anataka kushiriki katika kupika goli na hilo, kwa maoni yangu, ni njia ya kufunga magoli mengi."


Robin van Persie ndiye mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi ya Ligi Kuu ya England katika mwaka wa kalenda wa 2012 akiwa amefunga jumla ya magoli 27 ambayo alizifungia klabu za Arsenal na Manchester United.


Katika mechi ya jana, magoli mengine mawili ya Manchester United yalifungwa na Javier Herndandez 'Chicharito.

Mabingwa Man City walishinda 3-0 nyumbani dhidi ya Stoke City kupitia magoli ya Pablo Zabaleta, Edin Dzeko na penalti ya Sergio Aguero, ambaye baadaye aliumia misuli ya nyuma ya paja.

Southampton iliinuka kutoka katika ukanda wa kushuka daraja baada ya kupata sare dhidi ya Arsenal lakini walikosa bahati kutoondoka na pointi zote tatu katika mechi ambayo kikosi cha Arsene Wenger kilicheza ovyo.

Wenyeji walipata goli la kuongoza wakati Gaston Ramirez alipouwahi mpira uliozagaa na kufumua shuti lililomshinda kipa Wojciech Szczesny.

Lakini Arsenal walijibu mashambulizi kabla ya  mapumziko wakati Guly do Prado alipojifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa 'fri-kiki' iliyopigwa na Theo Walcott.


Dimitar Berbatov na Alex Kacaniklic walifunga wakati Fulham ilipopata ushindi wao wa pili tu ugenini dhidi ya timu inayotisha msimu huu ya West Brom.

Berbatov aliifungia timu yake goli la kuongoza kwa shuti la chini kabla ya Romelu Lukaku kusawazisha mara baada ya mapumziko kwa shuti la jirani na lango, ingawa picha za marudio zilionyesha alikuwa ameotea.

Lukaku na Zoltan Gera wote waligongesha miamba kwa upande West Brom.


Lakini Kacaniklic aliwapa wageni ushindi waliostahili kufuatia pasi tamu ya Bryan Ruiz. 


 

Msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya mechi zahjana



Nafasi Timu Mechi Goal Difference Pointi
1. Man Utd 21 26 52
2. Man City 21 22 45
3. Tottenham 21 12 39
4. Chelsea 19 21 38
5. Arsenal 20 18 34
6. Everton 20 8 33
7. West Brom 21 2 33
8. Swansea 21 5 29
9. Stoke 21 1 29
10. Liverpool 20 5 28
11. West Ham 20 0 26
12. Norwich 21 -10 25
13. Fulham 21 -5 24
14. Sunderland 20 -5 22
15. Newcastle 20 -11 20
16. Aston Villa 21 -24 19
17. Southampton 20 -11 18
18. Wigan 21 -17 18
19. Reading 21 -17 13
20.
QPR


20-2010

No comments:

Post a Comment