Wednesday, January 2, 2013

SAJUKI AFARIKI DUNIA

Marehemu Sajuki
Sajuki siku alipoanguka jukwaani Arusha

Marehemu Sajuki enzi akiwa na Wastara kabla ya ndoa yao


NYOTA wa filamu nchini, Juma Kilowoko 'Sajuki', amefariki dunia leo saa 12 asubuhi baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Muigizaji huyo amefariki katika hospitali ya taifa, Muhimbili, alipokuwa amelazwa kwa zaidi ya wiki moja.

Sajuki amefariki ikiwa ni siku kadhaa tu baada ya serikali kusema kwamba ingeenda kumtibia nchini India, ambako alienda awali kwa michango ya Watanzania na kupata nafuu kabla ya kurejewa tena na hali hiyo.

Hivi karibuni, Sajuki alianguka jukwaani baada ya kuishiwa na nguvu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ambako alishiriki tamasha maalum la kusaidia kukusanya fedha za kurejea kwenye matibabu nchini India.

Kwa mujibu taarifa za awali, msiba upo Tabata Bima nyumbani kwa marehemu, lakini wanasubiri maamuzi ya wazazi wake wanaoishi Songea kujua mazishi yatafanyikia wapi.

Msanii huyo alizushiwa kifo mara kadhaa kabla ya mauti kumkuta asubuhi ya leo.

Ndoa yake imekuwa na misukosuko ya kimaisha ambapo kabla ya kufunga ndoa na muigizaji mwenzake, Wastara, wawili hao walipata ajali ya pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Sajuki, ajali iliyosababisha mwanamke huyo kukatwa mguu.

Mungu ailaze roho ya marehemu Sajuki mahala pema Peponi. Amina.

No comments:

Post a Comment