Saturday, January 5, 2013

VAN MAGOLI AIOKOA MAN UNITED ISIADHIRIKE WEST HAM

Robin van Persie

ROBIN van Persie alifunga goli la dakika za majeruhi wakati Manchester United iliponusurika kutolewa katika michuano ya Kombe la FA kwa kulazimisha sare ya 2-2 na kuinyima West Ham ushindi wa kukumbukwa.

Tom Cleverley aliwafungia wageni goli la kuongoza wakati alipoutumbukiza mpira kwenye nyavu ndogo kabla ya James Collins kufunga goli la kusawazisha kwa kichwa lililokuwa goli lake la kwanza katika klabu hiyo.

Collins aliwapa uongozi wa 2-1 West Ham kwa goli jingine la kichwa lililofanana na la kwanza ambalo pia lilitokana na krosi ya mtu yule yule winga wao mpya, Joe Cole aliyejiunga jana akitokea Liverpool na kumuacha kipa David de Gea akiwa "amepigiliwa misumari" ardhini kama ilivyo kuwa katika goli la kwanza.

Huku sekunde zikiwa zinayoyoma baada ya kuongezwa dakika nne za majeruhi, Van Persie aliinasa kwa ufundi wa hali ya juu pasi ndefu kutoka kwa Ryan Giggs aliyeuwahi mpira uliopotezwa na mshambuliaji wa West Ham, Carlton Cole, na kumtengenezea muuaji huyo goli lake la 20 katika michuano yote msimu huu tangu ajiunge na Man United kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 24 akitokea Arsenal katika kipindi kilichopita cha usajili.

Matokeo hayo yanamaanisha kwamba sasa timu hizo zitarudiana Old Trafford.

No comments:

Post a Comment