Sunday, January 6, 2013

TUZO BALLON D'OR KESHO ANASTAHILI MESSI - AGUERO

Aguero (kushoto) akiwa na Lionel Messi katika timu ya taifa ya Argentina

SERGIO Aguero alihojiwa na gazeti la Argentina la 'Ole' na kusema kwamba tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia ya Ballon d'Or inapaswa kwenda kwa Lionel Messi. 

Sherehe za kumtangaza mwanasoka bora wa dunia wa mwaka 2012 zitafanyika kesho kwenye Ukumbi wa Zurich Convention Centre nchini Uswisi.

"Anastahili tuzo hiyo kwa yote aliyoyafanya akiwa na Barcelona na timu ya taifa ya Argentina," alisema Muargentina huyo, ambaye pia ana ndoto za kuja kuwa mchezaji bora wa dunia siku moja. "Si jambo rahisi, lakini kama utafanya mambo yako vizuri huwezi kujua (unaweza kushinda tuzo). Unajua daima unapaswa kuota kuwa mchezaji bora duniani," aliongeza.


Mshambuliaji huyo wa Manchester City pia alizungumzia kiwango cha timu yake cha sasa. "Hatujacheza kama ambavyo tulikuwa tukicheza msimu uliopita, lakini tuko katika nafasi nzuri. Tunaongezeka ubora na katika mechi mbili zilizopita tulicheza vizuri sana. Tuna kikosi kizuri na tuna uwezo wa kurejea katika kiwango kama cha msimu uliopita. Kutolewa kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ilikuwa pigo kubwa kwa sababu tulikuwa na matumaini makubwa katika michuno ile. Tulikuwa katika kundi gumu. Taji la Ligi ya Klabu Bingwa ni jambo tunaloliota pia. Tutafanya vyema siku zijazo," alisema.


Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina pia alijumuisha mwaka wake 2012 akisema: "Ulikuwa ni mwaka mzuri katika maisha yangu ya soka. Ulikuwa muhimu katika kujijenga kwenye klabu ya Man City na kutwaa ubingwa wa England. Na kikubwa ni kufunga goli lile lililoamua bingwa katika dakika za lala salama. Ilikuwa ni ndoto iliyogeuka kwa kweli," aliongeza Aguero.


Mshambuliaji huyo pia alizungumzia timu ya taifa ya Argentina, akisema: "Jambo muhimu zaidi ni kwamba tufuzu kwa Kombe la Dunia 2014 mapema iwezekanavyo. Kama ukipoteza mechi mbili katika michuano hii migumu ya kuwania kufuzu timu nyingine zinakufikia. Ulikuwa ni mwaka mzuri kwa timu ya taifa. Tumeanza kuzoeana na kufanya mambo sahihi uwanjani," alisema.

No comments:

Post a Comment