Monday, January 7, 2013

RONALDO SHUJAA REAL MADRID WAKIMALIZA 10 UWANJANI

Ronaldo akishangilia baada ya kufunga dhidi ya Real Sociedad
Ronaldo akienda kumkumbatia kocha wake Jose Mourinho baada ya kutupia goli

Kipa wa Real Madrid, Antonio Adan (kulia) akitolewa kwa kadi nyekundu
Iker Casillas akiingia uwanjani baada ya Adan kula 'red'
Goooooooooo! Huyu ndiye Ronaldo tunayemfahamu.... Cristaiano akifunga goli lake la pili jana kwa 'fri-kiki' ya hatari

MAGOLI, kadi nyekundu 2 na kuzomewa kwa kocha Jose Mourinho na mashabiki wao, ni mambo yaliyotawala mechi ya jana usiku ya La Liga ambayo Real Madrid walishinda 4-3 dhidi ya Real Sociedad huku straika Cristiano Ronaldo akiibuka shujaa wa timu yake kwa kufunga magoli mawili wakati wakiwa wamebaki 10 uwanjani.

Real Madrid walionekana kama wanauanza Mwaka Mpya vibaya wakati Mourinho alipomuacha benchi kwa mara ya pili mfululizo nahodha Iker Casillas na kumweka langoni Antonio Adan, ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu mapema katika dakika ya sita baada ya kumuangusha ndani ya boksi mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Carlos Vela na kusababisha penalti.

Casillas aliingia langoni na kufungwa penalti iliyotokana na kosa hilo kupitia kwa Xabi Priet, ambaye pia alikuwa na usiku mzuri jana baada ya kumtungua 'hat-trick' Casillas.

Hata hivyo, magoli mawili kutoka kwa Karim Benzema, Sami Khedira na mawili ya Ronaldo yalimuepushia aibu ya kufungulia mwaka Mourinho ambaye alikuwa akizomewa mashabiki wake kutokana na kumpanga Adan langoni badala ya Casillas.

Real ndio walioanza vizuri mechi na kupata goli la kuongoza katika dakika ya 2 tu ya mechi kupitia kwa Benzema akitumia pasi ya Khedira. Dakika chache baadaye kipa Adan alitolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea faulo Vela ndani ya boksi. Wakati Casillas akiingia kutokea benchi mashabiki wa Real waligawanyika kwa wengine kumshangilia huku wengine wakimzomea kutokana na hali ya sasa. Xabi Prieto alisawazisha kupitia penalti hiyo.

Kisha Khedira akafunga kwa kisigino goli la pili la Real Madrid (2-1) kabla ya Xabi Prieto kusawazisha (2-2) kabla ya mapumziko.

Cristiano Ronaldo, ambaye alipewa kitambaa cha unahodha kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo, alionyesha umuhimu wake kwenye timu wakati alipocheza kwa kiwango cha juu katika kipindi cha pili.

Kwanza, Mreno huyo aliiwahi pasi ya Benzema na kufunga goli la tatu la Real Madrid (3-2) kabla ya kufunga la nne (4-2) kwa 'fri-kiki' ya hatari iliyogonga chini ya besela baada ya kipa Bravo kuigusa kidogo na kutinga wavuni.

Xabi Prieto alikamilisha 'hat-trick' yake kwa kuifungia Sociedad goli la tatu (4-3) kwa shambulizi la kustukiza dakika chache kabla ya mchezaji wao Estrada naye kutolewa kwa kadi ya pili ya njano na kuzifanya timu zote mbili kumaliza zikiwa na wachezaji 10 kila moja uwanjani.

No comments:

Post a Comment