Tuesday, January 15, 2013

TAZAMA MAPICHA KIBAO YA MAANDAMANO YA WANAFUNZI CHUO CHA USIMAMIZI WA FEDHA (IFM) JIJINI DAR ES SALAAM KULAANI POLISI KWA KUSHINDWA KUCHUKUA HATUA DHIDI YA VITENDO VYA UPORAJI NA ULAWITI WANAVYOFANYIWA KILA UCHAO... KAMDNA KOVA AINGILIA KATI NA KUMBANA RPC WA TEMEKE ALIYEISHIA KUJIBU KUWA ETI, WALIKUWA WAKISIKIA JUUJUU TU NA KWAMBA HAWANA TAARIFA RASMI... FFU NAO WAWAGEUZIA KIBAO BAADHI YA MADENTI NA KUWATEMBEZEA KICHAPO BILA HURUMA!


Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),  jana walifanya maandamano makubwa jijini Dar es Salaam hadi katika Makao Makuu ya  Polisi na Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakililalamikia Jeshi hilo kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya wizi na kulawitiwa wanavyofanyiwa na genge la watu katika hosteli iliyoko Kigamboni.

Mamia ya wanafunzi hao walianza kuandamana kutoka chuoni kwao katikati ya Jiji  saa 4:40 asubuhi na kuwasili makao makuu ya Jeshi hilo ambayo yapo pia makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi saa 5:33 asubuhi.

Baada ya kuwasili, walisema dhumuni la maandamano yao ni kutaka kuonana na Mkuu wa Polisi  (IGP), Said Mwema au Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ili kufikisha kilio chao kwao.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa IFM, Michael Charles, alisema wanafunzi wamekuwa wakivamiwa na kuibiwa mali zao ikiwamo kompyuta ndogo (laptop), kubakwa na kulawitiwa katika hosteli ya Kigamboni wilayani Temeke.

Charles alisema licha ya matukio hayo kuripotiwa  katika kituo cha polisi Machava kilichopo Kigamboni, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi na hivyo kuwafanya wanafunzi wahisi kuwa huenda vitendo hivyo vina baraka za polisi.

“Juzi tulivamiwa na wenzetu wawili wakapigwa mapanga, tukaibiwa kompyuta na wenzetu wengine wakalawitiwa, ndiyo maana tumeamua kuandamana kupeleka malalamiko yetu kwa sababu  tumeona kinachofuata tunaweza kuuawa,” alisema Charles.

Charles alisema mpaka sasa idadi ya komputa za wanafunzi zilizoibwa ni 300 ambazo zimekuwa zikiibwa kila siku.

Awali  baadhi ya wanafunzi walizuiliwa eneo la jengo la PPF wasifike Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, wanafunzi hao walikwama kuonana na IGP Mwema na Dk. Nchimbi baada ya kuzuiliwa na maafisa wa jeshi hilo katika lango kuu la kuingilia badala yake na walielezwa na askari waliokuwa langoni hapo kuwa wachague watu watatu ili waruhusiwe kwenda kuonana na viongozi hao.

Jitihada zilizofanywa na maafisa wa polisi H. Mbezi na N. Marijan, kuwataka wachague wenzao watatu kwenda kutoa malalamiko yao ziligonga mwamba kufuatia baadhi ya wanafunzi hao kudai kwa wanaovyoifahamu polisi, wale watakaokwenda huko watawekwa chini ya ulinzi na suala lao halitasikilizwa tena.

Baadaye wanafunzi hao walibadilisha maelezo kwa kudai kuwa wanataka kuonana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ili wamweleze kilio chao.

Ilipofika saa 6:03 mchana, Kova aliwasili Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kuzua shangwe kubwa kutoka kwa wanfunzi hao ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu kwamba huyo ndiye atakayeweza kuwasikiliza kilio chao na kukipatia ufumbuzi.

Kova baadaye alizungumza na wanafunzi hao kwa kuwataka afuatane nao hadi Kigamboni ili watuhumiwa wa vitendo hivyo wakamatwe haraka.

Msafara wa Kova ambaye alikuwa katika gari namba PT 1574 pamoja na Charles na Waziri Mkuu wa IFM aitwaye Mangesho, ulianza safari ya  kuelekea Kigamboni  saa 6:11 mchana, huku ukifuatana na mamia ya wanafunzi wa chuo hicho.

 Hata hivyo, hali ilikuwa mbaya zaidi  baada ya idadi kubwa ya wanafunzi hao kutaka kuvuka katika kivuko eneo la Ferry na hivyo kuulazimu uongozi wa kivuko hicho kusimamisha safari ili kupunguza wengine.

Halikuwa jambo rahisi kuwapunguza wanafunzi hao katika kivuko na hivyo kusababisha mabishano yaliyochukua muda mrefu  kati ya uongozi wa kivuko, Jeshi la Polisi likiongozwa na Kova pamoja na wanafunzi hao ambao walikuwa wanagoma kupunguzwa. 

Mabishano hayo yalidumu kwa zaidi ya saa tatu hadi walipokubaliana kusafirishwa kwa awamu.

"Kitaalamu hatuwezi kuondoa kivuko kwa sababu idadi ya watu ni kubwa na hilo haliruhusiwi, labda wengine wapunguzwe,” alisema Mhandisi wa Mambo ya Bahari, Reuben Materu.

Kwa upande wake, Kova alisema: “ Hili jambo halihitaji ushabiki. Ni la kiutaalamu zaidi, tunaweza kuwaruhusu wavushwe hivyo hivyo, lakini ikaleta madhara mengine makubwa zaidi.”

 Mabishano hayo yalizuia safari za abiria wengine hadi wanafunzi wote waliposafirishwa kwa awamu.

POLISI WAFYATUA MABOMU
Licha ya wanafunzi kukubaliana na Polisi kuelekea katika Uwanja wa Machava, lakini baadhi ya wanafunzi walidaiwa kukiuka makubaliano hayo baadaye na  kuelekea kituo cha polisi cha Kigamboni huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kulaani Jeshi la Polisi na kuona hivyo, askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakafyatua mabomu ya machozi kwa takribani dakika 20.

 Mbali na kufyatua mabomu, pia waliwakamata wanafunzi zaidi ya 100 na kuwapeleka katika kituo cha polisi Kigamboni, lakini baadaye waliachiwa na kuelekea sehemu ya uwanja kwa ajili ya mazungumzo na Kova.
Baadhi ya wananchi wa  Kigamboni walijitokeza kutoa ushuhuda, akiwamo kijana mmoja aliyesema:

“Ni kweli wanafunzi huwa wanaibiwa. Ninawafahamu hao wezi na kama mkitaka nitawapeleka.” 

Symphorasa Ndyamukama, mkazi wa Kigamboni na mmoja wa wamiliki wa hosteli za wanafuzni hao, alisema alishawahi kutoa taarifa hizo za uhalifu polisi, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kukomesha vitendo hivyo.

 Kutokana na hali hiyo, Kova ambaye alikuwa amefuatana na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alimtaka atoe ufafanuzi juu ya taarifa hizo.

Kamanda Kiondo alijibu kwamba taarifa hizo za uhalifu hazijawahi kuripotiwa polisi rasmi isipokuwa walikuwa wanazisikia tu.

Kutokana  na hali hiyo, Kamanda Kova alimuagiza Kiondo kulifanyia kazi  mara moja suala hilo ili kubaini wahalifu na kuwakamata.

Alisema vilevile kuwa atamteua askari atakayeshirikiana naye katika kuwabaini wahalifu katika eneo hilo, na kuagiza zoezi hilo kuanza jana mara moja.

No comments:

Post a Comment