Tuesday, January 15, 2013

GERVINHO ATUPIA 2 IVORY COAST IKIUA MISRI

Gervinho a.k.a KaziBure

MSHAMBULIAJI wa Arsenal, Gervinho a.k.a KAZIBURE, alifunga mara mbili na kuisaidia timu yake ya taifa ya Ivory Coast kushinda 4-2 katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Misri ya kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika iliyofanyika Abu Dhabi jana usiku.

Ivory Coast waliruhusu goli la kichwa kutoka kwa Mohamed Aboutrika katika dakika ya 18 lakini walirejea mchezoni baada ya Gervinho kufunga penalti.

Goli la mshambuliaji mrefu wa Anzhi Makhachkala, Lacina Traore, wa Ivory Coast lilibadili mwelekeo wa mechi kabla ya Gervinho kufunga goli lake la pili na la tatu kwa timu yake muda mfupi baada ya mapumziko.

Mohamed Nagui 'Gedo' aliwafungia Mafarao goli jingine moja katika dakika ya 60 lakini lilionekana kama la kujiliwaza tu kwani Didier Ya Konan aliifungia Ivory Coast goli la nne dakika nane kabla mechi haijamalizika.

Ivory Coast, ambayo iko katika Kundi D, itacheza mechi yake ya ufunguzi wa AFCON dhidi ya Togo mjini Rustenburg, Afrika Kusini Januari 22.

No comments:

Post a Comment