Wednesday, January 2, 2013

AGUERO SHAKANI KUIVAA ARSENAL

Aguero akiugulia baada ya kuumia misuli jana

MANCHESTER City wanahofu kwamba Sergio Aguero atakosa mechi yao muhimu ugenini dhidi ya Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates Januari 13 kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma ya paja.

Mshambuliaji huyo mwenye thamani ya paundi milioni 38 alitoka akichechemea baada ya kufunga kwa penalti katika ushindi wa Man City wa 3-0 dhidi ya Stoke katika Siku ya Mwaka Mpya.

Muargentina huyo atakosa mechi ya Jumamosi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Watford.

"Ni vigumu kutambua ukubwa wa tatizo kama lile haraka lakini kwa uzoefu wangu yuko shakani kucheza dhidi ya Arsenal," alisema kocha msaidizi David Platt.

"Kutakuwa na uvimbe mkubwa na kuvuja damu kidogo lakini hatuwewzi kujua ndani ya saa 48 atakuwa nje kwa muda gani."

Mechi dhidi ya Arsenal ndiyo inayofuatia kwa Man City katika Ligi Kuu ya England na inakuja siku siku moja na vinara Manchester United - ambao wako juu yao kwa tofauti ya pointi saba - wataikabili Liverpool katika mechi nyingine muhimu kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Kocha wa Man City, Roberto Mancini alijaribu kupuuza jeraha hilo akiongeza: "Sidhani kama ni kubwa. Msuli wake wa nyuma ya paja unauma, pengine ndani ya siku 10 atakuwa amepona."

Aguero ndiye kinara wa magoli wa Man City akiwa na magoli 10, sawa na Edin Dzeko ambaye pia alifunga dhidi ya Stoke jana.

Wawili hao wamefunga magoli matano kati ya saba yaliyofunngwa na Man City katika mechi zao mbili zilizopita, baada ya pia kusaidia timu yao kushinda 4-3 dhidi ya Norwich Jumamosi.

Kukoseka kokote kwa muda kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kutakuwa ni pigo jingine kwa Mancini, ambaye atamkosa kiungo wake muhimu Yaya Toure kwa Januari nzima.

Yaya Toure alicheza dakika 90 dhidi ya Stoke lakini pamoja na kaka yake, beki Kolo, watajumuika na kikosi cha Ivory Coast kwa ajili ya fainali za Mataifga ya Afrika na anaweza kuwapo nchini Afrika Kusini kwa muda wa kufikia wiki sita.

"Haijalishi kama Yaya ataondoka ama vipi," aliongeza Platt. "Changamoto ni kuendelea kushinda mechi.

"Tuna kikosi cha wachezaji ambacho tunahitaji kuchagua 11 kutoka humo. Wachezaji 11 woeote tutakaowashusha uwanjani, tunatarajia waende kuchukua pointi."

Habari njema kwa Man City ni kurejea katika uzima kwa Mario Balotelli, ambaye hakucheza mechi mfululizo za mwisho wa mwaka kutokana na kusumbuliwa na virusi.

"Mario amerejea mazoezini kwa siku mbili ama tatu zilizopita," Platt alifafanua.

"Inaonekana kama amelishinda tatizo sasa. Tatizo alilokuwa nalo ni kwamba alikuwa mgonjwa, akarejea na kufanya mazoezi na kisha akaugua tena.

"Inaonekana amepona kikamilifu sasa na ana siku nyingine kama tatu kabla ya mechi dhidi ya Watford wikiendi hivyo kuna nafasi kubwa kwamba atacheza Jumamosi."

No comments:

Post a Comment