Pedro akishangilia moja ya magoli yake dhidi ya Espanyol jana usiku |
Messi akifunga penalti dhidi ya Espanyol jana usiku |
Iniesta akimpongeza Xavi baada ya kufunga jana |
Kocha Tito Vilanova wa Barcelona akiiongoza timu yake jana, siku 17 tu baada ya kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutibiwa saratani ya koo |
Thiago Alcantara (kulia) akimiliki mpira baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Xavi aliyepumzishwa baadaye jana |
BARCELONA waliuanza mwaka 2013 kama walivyoumaliza 2012, wakitawala mchezo kwa hali ya juu na 'kuimaliza' mechi iliyotarajiwa kuwa ngumu kutokana na upinzani wa jadi dhidi ya mahasimu wa mji mmoja, Espanyol, ndani ya dakika 28 tu za kwanza baada ya kufunga magoli manne katika ushindi wa 4-0 jana usiku.
Espanyol ambao ni wa tatu kutoka mkiani, walidhaniwa wangewapa wakati mgumu Barcelona lakini haikuonekana kama mechi ya wapinzani wa jadi na badala yake wageni walitumia usiku mzima kuusaka mpira kwa tochi.
Lionel Messi alifunga goli lake la 26 katika ligi msimu huu kwa njia ya penalti, Pedro (mawili) na Xavi Hernández walikamilisha ushindi wa kujiamini, ambao ungeweza kuwa mkubwa zaidi kama magoli mawili waliyofunga kipindi cha pili yaliyoonekana kuwa ya halali yalipokataliwa kwa madai ya kuotea.
Xavi alifungua milango ya wageni katika dakika ya 10 baada ya pasi nyingi za kuhama kutoka upande mmoja hadi mwingine kabla ya mpira kukumkuta Iniesta kwenye wingi ya kushoto ambaye aliurudisha ndani mpira kwa Xavi ambaye alifunga kiulaini.
Dakika sita baadaye, Barca walikuwa wakiongoza 2-0 kufuatia gonga nyingine nyingi. Cesc Fabregas alimpiga chenga beki, akakimbia kuelekea langoni, akampasia Messi ambaye naye alipiga shuti lililokuwa kilielekea nje lakini Pedro aliligusa kidogo kwa goto na mpira ukatinga wavuni.
Pedro akafunga tena goli lake la pili jana na kufanya matokeo yawe 3-0 baada ya kuiwahi pasi ya Sergio Busquets na kuuchota mpira juu ya kipa Kiko Casilla -- kwa staili ya ufungaji ya Messi.
Barca walifunga goli la nne kwa penalti katika dakika ya 28 kupitia kwa Leo Messi, baada ya Fabregas kuangushwa na kipa ndani ya boksi.
Messi ambaye leo jioni anapewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo yake ya nne mfululizo ya Ballon d'Or ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa mwaka 2012, licha ya kuanza mwaka na goli hakucheza vizuri -- bila ya shaka akili yake ilikuwa kwenye ukumbi wa Ukumbi wa Convention Centre mjini Zurich, Uswisi, ambako sherehe za tuzo hizo zitafanyika. Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Messi kucheza chini ya kiwango katika mechi ya kuamkia siku ya tuzo hizo. Bila ya shaka anawaza itakuwaje huko Uswisi.
No comments:
Post a Comment