Tuesday, January 8, 2013

REAL MADRID KONA 133 MAGOLI "0"


SIFURI kwenye 133 inaweza kuonekana kama takwimu za mitupo huru ya Shaquille O’Neal au Dwight Howard kwenye mchezo wa kikapu. Badala yake hiyo ni takwimu ya kikosi cha kocha Jose Mourinho cha ReaI Madrid kwenye kona walizopiga msimu huu.

Real Madrid ndiyo timu iliyopiga kona nyingi zaidi katika La Liga na haijafunga goli hata moja, kama zilivyo timu tano za chini kwenye msimamo zinazopigania kutoshuka daraja za Mallorca, Celta Vigo, Osasuna, Zaragoza na Rayo Vallecano.

Kabla ya mechi ya Jumapili, Madrid walikuwa wamepiga kona 133 katika mechi 17 – wastani wa zaidi ya kona 7 kwa kila mechi – na hawajafunga goli hata moja. Getafe, tayari wamefunga magoli manne katika kona 29 pungufu ya Real Madrid.

Inaonekana ni tatizo ambalo halijapatiwa ufumbuzi na inazua maswali inawezekanaje kwa timu yenye wapigaji kona bora kama Ozil, Kaka, Modric, Xabi Alonso au Di Maria na wapiga vichwa wenye vipaji kama Sergio Ramos, Pepe, Khedira au Cristiano Ronaldo, haijafunga goli hata moja kutokana na kona.

Mourinho si kwamba ameachwa nyuma kwenye ligi kutokana na kushindwa kufunga kona tu bali kwa sababu timu yake inashindwa pia kuzuia kona. Real Madrid imefungwa kwa kona sita msimu huu, na hivyo kudondosha pointi 10 kati ya 18 walizopoteza kufikia sasa msimu huu.

"Hatuwezi kuongeza juhudi zaidi ya kujifua katika mipira ya adhabu ndogo", Mourinho alisema. Kwa kuongeza juhudi ama kwa kutoongeza, Real Madrid ni lazima iongeze ubora kwa sababu Manchester United wanawasubiri jirani kwenye kona.

No comments:

Post a Comment