Thursday, January 24, 2013

REAL MADRID, BARCELONA VINARA WA LIGI YA ‘MIHELA’ DUNIANI… ZINAFUATIWA KWA MBALI NA MANCHESTER UNITED, BAYERN MUNICH, CHELSEA, ARSENAL


Uwanja wa Santiago Bernabeu unaomilikiwa na Real Madrid.

Uwanja wa Santiago Bernabeu

Uwanja wa Camp Nou unaomilikiwa na Barcelona.

Uwanja wa Camp Nou.

LONDON, England
REAL Madrid na mahasimu wao wa jadi, Barcelona walithibitisha kwamba mapenzi kwa soka la Hispania hayajatetereka licha ya hali mbaya ya kifedha, wakijichimbia kileleni mwa klabu zinazoingiza fedha nyingi zaidi duniani, kampuni ya huduma za biashara ya Deloitte imesema katika taarifa yake leo. 

Real, ambayo ilitwaa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania mwezi Mei ikiwa ni mara yao ya 32 kufanya hivyo, imeandika rekodi kwa kuwa klabu ya kwanza ya mchezo wowote ule duniani kuingiza mapato ya zaidi ya euro milioni 500 (Sh. trilioni moja)  kwa mwaka, kwa mujibu wa taarifa ya mwaka ya Deloitte kupitia kile wanaochoita ‘Ligi ya Fedha katika Soka  2011-12’. 

Mahasimu wa jadi katika soka la Hispania wamedumisha hali yao ya kupata uungwaji mkono wa kiasi kikubwa kutoka kwa mashabiki wao, wakijaza watu wanaozidi 80,000 katika kila mechi kwenye viwanja vyao licha ya kuyumba kwa uchumi wa Hispania na kuongezeka kwa tatizo la ukosefu wa ajira.
Uwapo wa mashabiki wao katika maeneo mbalimbali duniani kote pia kumewasaidia kusaini mikataba minono ya udhamini wa kimataifa. 

Vigogo hao wa Hispania wananufaika vilevile na utaratibu unaowaruhusu kuingia makubaliano binafsi ya haki za kurushwa mechi zao kwenye televisheni badala ya kufanya hivyo kwa pamoja na klabu nyingine kama ilivyo kwa mahasimu wao wakuu wa nchi nyingine za Ulaya.
Athari za ‘ubabe’ huo wa Real na Barca ni kwamba, zinadhoofisha soka la Hispania kwani klabu nyingine nyingi zinahaha kiuchumi. 

Manchester United ya England iko ya tatu nyuma nyuma ya vigogo hao wa Hispania licha ya kuanguka msimu uliopita baada ya kukosa kombe lolote kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2005.
Bayern Munich ya Ujerumani inakamata nafasi ya nne, ikifuatiwa na mabingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, Chelsea na mahasimu wao katika Ligi Kuu ya England, Arsenal. 

"Kutobadilika kwa orodha ya 6-bora kunadhihirisha ukweli kwamba klabu hizi zina mashabiki wengi zaidi na hivyo kuwa na mapato makubwa kuliko wengine, kwa masoko yote ya ndani ya nchi zao na pia kimataifa," amesema Dan Jones, mmoja wa maafisa wa biashara katika michezo kwenye kampuni ya Deloitte.

LIGI 5 BORA
Kwa ujumla, mapato ya klabu 20 yamepanda kwa asilimia 10 hadi kufikia euro bilioni 4.8 mwaka 2011-12, kuonyesha kwamba ni kwa namna timu kubwa za Ulaya bado zimekuwa zikidai malipo makubwa kutoka kwenye kampuni za TV na kampuni zinazowadhamini licha ya hali ngumu iliyopi ya kiuchumi. 

Klabu za juu 20 ndizo zilizovuna zaidi ya robo ya mapato yote ya soka katika soko la Ulaya, kudhihirisha pengo kubwa lililopo baina ya tajiri na maskini katika mchezo huo. 

Taarifa ya Deloitte imejumuisha klabu zote za soka duniani lakini klabu zote zilizomo katika ‘top 20’ zinatoka katika ligi kuu tano tu za Ulaya, huku England ikiongoza kwa kutoa timu saba. 

AC Milan, inayomilikiwa na waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi, ndiyo inayoongoza miongoni mwa klabu tano za Italia, wakati Ujerumani ikitoa timu nne na Ufaransa timu mbili.
Mabingwa wa England, klabu ya Manchester City inayotegemea fedha kutoka kwa mmiliki wake kutoka Abu Dhabi, imeonyesha kuwa na mapato makubwa zaidi kufuatia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 44. Man City imekuwa ikivuna fedha nyingi kutokana na mkataba wa udhamini walioingia na kampuni ya Etihad Airways. 

KLABU ZINAZOONGOZA ‘TOP 20’
1. Real Madrid (Hispania)        Sh. trilioni 1.084
2. Barcelona   (Hispania)        Sh. trilioni 1.021
3. Man U       (England)         Sh. bilioni 837
4. Bayern      (Ujerumani)       Sh. bilioni 779
5. Chelsea     (England)         Sh. bilioni 682
6. Arsenal     (England)         Sh. bilioni 614
7. Man City    (England)         Sh. bilioni 604
8. AC Milan    (Italia)          Sh. bilioni 543
9. Liverpool   (England)         Sh. bilioni 493
10. Juventus   (Italia)          Sh. bilioni 413
11. Dortmund   (Ujerumani)       Sh. bilioni 400
12. Inter      (Italia)          Sh. bilioni 393
13. Tottenham  (England)         Sh. bilioni 377
14. Schalke    (Ujerumani)       Sh. bilioni 369
15. Napoli     (Italia)          Sh. bilioni 314
16. Marseille  (Ufaransa)        Sh. bilioni 287
17. Lyon       (Ufaransa)        Sh. bilioni 279
18. Hamburg    (Ujerumani)       Sh. bilioni 256
19. AS Roma    (Italia)          Sh. bilioni 245
20. Newcastle  (England)         Sh. bilioni 243


No comments:

Post a Comment