Wednesday, January 2, 2013

NEWCASTLE WAIKUBALIA CHELSEA KUMSAJILI DEMBA BA MWEZI HUU...!


Demba Ba
LONDON, England
Newcastle United wamewapa ruhusa mabingwa wa Ulaya, Chelsea kufanya mazungumzo na straika wao mwenye miaka 27, raia wa Senegal Demba Ba ili ikiwezekana wamsajili katika kipindi cha uhamisho wa dirisha dogo kilichoanza jana.

"Chelsea wametuma ombi rasmi la kumtaka Demba Ba na wako tayari kuvunja mkataba wa mchezaji huyu," Newcastle wamesema jana kupitia tovuti yao (www.nufc.co.uk).

"Klabu imemruhusu pia mchezaji kuzungumza na Chelsea na hivyo hatakuwamo katika kikosi chetu kitakachocheza leo (mechi ya ligi kuu) dhidi ya Everton."

Newcastle, wanaoshika nafasi ya sita kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi, hawakueleza zaidi kuhusiana na gharama za kuvunja mkataba wa Ba lakini vyombo vya habari vimefichua kuwa ni takriban paundi za England milioni 7 (Sh. bilioni 18).

Ba amekuwa nguzo katika safu ya ushambulaiji ya Newcastle tangu atue akiwa huru kutoka West Ham United, Juni 2011.

Straika huyo, ambaye alishawahi pia kuzichezea Rouen, Mouscron na Hoffenheim, alihitaji kucheza mechi nane kabla ya kufunga goli lake la kwanza Newcastle lakini alimaliza ukame wake kiaina kwa kupiga 'hat-trick' wakati walipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Blackburn Rovers.

Ba alimaliza msimu wa 2011-12 akiwa kinara wa mabao katika klabu ya Newcastle baada ya kufunga magoli 16, ikiwamo hat-trick nyingine dhidi ya Stoke City.

Ameendelea na makali yake ya kupachika mabao msimu huu, akifunga magoli 13 katika Ligi Kuu ya England, akishika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji inayoongozwa na straika wa Manchester United mwenye mabao 16, Robin van Persie.

Chelsea wamepania kupata msaidizi wa straika wao wa kimataifa wa Hispania, Fernando Torres ambaye ndiye amekuwa mchezaji anayecheza zaidi msimu huu kufuatia kubaki peke yake baada ya kuondoka kwa Didier Drogba na Salomon Kalou mwanzoni mwa msimu na pia kutolewa kwa mkopo kwa Romelu Lukaku kwenda klabu nyingine ya ligi kuu ya West Bromwich Albion.

No comments:

Post a Comment