Saturday, January 26, 2013

MESSI YUKO POA, KOCHA BARCA AFAFANUA

Lionel Messi

TAARIFA zilizagaa kwamba Barcelona inajiandaa kucheza mechi ya wikiendi hii bila ya straika wao Lionel Messi, baada ya mwanasoka bora wa dunia huyo kupumzishwa katika dakika ya 82 katika mechi yao waliyoshinda 4-2 dhidi ya Malaga katika robo-fainali ya Kombe la Mfalme Alhamisi.

Hata hivyo, kocha msaidizi wa Barcelona, Jordi Roura, ambaye alimpumzisha Muargentina huyo juzi, amesema Messi yuko poa.

Roura aliiambia tovuti ya fcbarcelona.com: "Tulimtoa Messi kama mbinu ya kumlinda. Maumivu kidogo kwenye mguu wake wa kulia yalikuwa yanampa shida. Lakini hana tatizo lolote kubwa."

Messi alifunga goli la nne la Barcelona katika ushindi huo wa 4-2 ugenini ambao uliipeleka Barca kwenye nusu fainali ya Kombe la Mfalme kwa ushindi wa jumla wa 6-4.

Magoli mengine ya Barca yalifungwa na Pedro, Iniesta na "baba Milan" Gerard Pique aliyekuwa akisherehekea kupata mtoto wake wa kwanza na muimbaji Shakira.

No comments:

Post a Comment