Tuesday, January 29, 2013

BILIONEA ALONGA: HENRY ANANISUKUMA NIMALIZIE KUNUNUA HISA ZOTE ARSENAL... NATAKA KUNUNUA MASTAA WAKUBWA, BODI INANIBANIA

Bilionea wa Arsenal, Alisher Usmanov

Thierry Henry

MWANAHISA mkuu wa Arsenal, Alisher Usmanov amesema kwamba mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo Thierry Henry "anamsukuma" amalizie kununua hisa zote za klabu hiyo ili aimiliki kikamilifu.

Henry hafurahishwi kuona timu hiyo kubwa haina kombe hata moja katika miaka saba, huku bodi ya klabu ikiwa ndiyo chanzo cha ubahili huku ikipingana na sera za Usmanov ambaye amesema yuko tayari kumwaga pesa kuibadilisha timu hiyo.

Usmanov yuko tayari kumwaga pesa kama Roman Abramovich afanyavyo Chelsea ili kurejesha heshima ya Arsenal na utayari wake unaonekana kuwavutia mashabiki ambao hawana furaha na sera za sasa usajili.

"Kwangu mimi, Arsene Wenger ni mmoja wa makocha bora kabisa duniani lakini inamuwia vigumu kufanya kazi yake," alisema Usmanov. "Nadhani anastahili kuwezeshwa kuwapata wachezaji bora wanaohitajika. Kama hilo litafanyika, tunaweza kumbana kwa kila jambo. Lakini kwa sasa, anatolewa kafara kwa sababu ya sera za klabu.

"Kila kitu hivi sasa kiko katika mikono ya (mwanahisa mwingine) Stan Kroenke. Natumai atafanikiwa, licha ya kwamba haendani na sera zangu. Mafanikio pekee makubwa kwa Arsene Wenger hivi sasa ni kuweza kutengeneza timu mbili: moja ambayo inapambana na mahasimu wetu na nyingine ya kujaribu kubaki kuwa bora kwenye ligi.

"Ndiyo maana nasema hiyo haitoshi kumbana kocha ila kwa kumpa pesa ya kununua 'masupastaa'. Na siyo 'masupastaa' tu, bali wale waliochaguliwa na Wenger.”

Licha ya nia yake ya kutaka kutaka kuibadili timu hiyo, Usmanov amekuwa akisukumwa kando na bodi ya Arsenal.

Bodi hiyo imekomalia kubaki katika kanuni za udhibiti wa fedha za UEFA za "Financial Fair Play", mbinu ambayo ni tofauti na mipango ya Usmanov.

"Arsenal hawaonyeshi kunihitaji. Mimi ni mtu ngangari. Kama mtu anahitaji sapoti yangu, pesa zangu, ujuzi wangu, daima niko tayari," alisema Usmanov.

No comments:

Post a Comment