Thursday, January 31, 2013

MESSI AWASHIANA NA ARBELOA KWENYE MAEGESHO BAADA YA SARE YA CLASSICO

Lionel Messi (kushoto) wa Barcelona akiwania mpira dhidi ya Michael Essien wa Real Madrid wakati wa mechi yao ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania jana usiku Januari 30, 2013. Timu hizo zilitoka 1-1.
Cristiano Ronaldo wa Real Madrid akipiga kichwa mpira wakati wa mechi yao ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya Barcelona kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania jana usiku Januari 30, 2013.

NYOTA wa Barcelona, Lionel Messi alibwatukiana na Alvaro Arbeloa katika maegesho ya magari ya Real Madrid jana usiku, imebainishwa.

Gazeti la Punto Pelota limesema wawili hao walichezeana undava wakati wote wa mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme iliyomalizika kwa sare ya 1-1 jana usiku.

Baada ya mechi, wakati Messi akielekea kwenye basi la timu ya Barcelona, alimuona Arbeloa katika gari lake akiwa na mkewe na kwa mara nyingine akambwatukia beki huyo wa kulia wa Real.

Arbeloa alijibu mashambulizi kabla ya Messi kuondolewa na mfanyakzi wa Barca kupelekwa kwenye basi.

Aidha, wachezaji wa Real kwenye chumba cha kuvalia hawakufurahishwa na tabia ya Messi wakati wa mechi hiyo. Wakati fulani, Messi, aliyekuwa ameangushwa, alikataa mkono wa kumuinua chini aliopewa na Xabi Alonso jambo lililowakera wachezaji wa Real.

Barcelona walitawala mechi lakini wageni hao kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu waliambulia sare tu kutoka kwa Real Madrid.

Timu zote mbili zilikuwa na nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza lakini goli la kuongoza halikuja hadi dakika tano baada ya mapumziko wakati Cesc Fabregas alipokimbilia pasi ya kupenyezewa na Lionel Messi na kumtungua kipa mpya Diego Lopez aliyesajiliwa Januari kuziba pengo la nahodha Iker Casillas ambaye atakuwa nje wa wiki sita kutokana na kuumia kidole.

Real walisawazisha dakika tisa kabla ya mechi kumalizika wakati mchezaji aliyeng'aa zaidi kwenye mechi hiyo beki yosso Raphael Varane (18) aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya Classico aliporuka juu na kufunga kwa kichwa kufuatia krosi ya Mesut Ozil. Timu hizo zitarudiana Jumatano ya Februari 27 kwenye Uwanja wa Nou Camp wa Barcelona.

No comments:

Post a Comment