Monday, January 7, 2013

LAMPARD ANAONDOKA CHELSEA MWISHO WA MSIMU, WAKALA WAKE ATHIBITISHA

Frank Lampard


FRANK Lampard hatapewa mkataba mpya klabuni Chelsea wakati mkataba wake wa sasa utakapomalizika Juni, wakala wake amethibitisha.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye goli lake alilofunga wikiendi limemfanya abakishe magoli 10 kuwa mfungaji bora wa muda wote Chelsea, ameshuhudia hatma yake ikiwekwa njiapanda mwezi huu, huku klabu za LA Galaxy, Lazio na Manchester United zikisemekana kudhamiria kumsajili.

Hata hivyo, wakala wa Lampard, Steve Kutner amebainisha kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa England aliambiwa wakati wa fainali za Kombe la Dunia la Klabu Desemba mwaka jana kwamba ataondoka klabuni hapo mwisho wa msimu huu.

"Wakurugenzi wa Chelsea walimweleza Frank hilo nchini Japan wakati wa Kombe la Dunia la Klabu kisha wakamsisitizia tena baada ya ushindi dhidi ya Everton kwamba hakuna namna yoyote itakayomfanya aongezwe mkataba wa kubaki klabuni mwisho wa msimu huu," Kutner aliliambia gazeti la The Daily Mirror.

"Hakuna kilichobadilika katika suala hilo.

"Frank amelazimika kukubali na anataka kucheza mpira Chelsea kwa juhudi zote ili amalize msimu akiwa na mafanikio kwa kadri iwezekanavyo kwa klabu anayoipenda."

Lampard amekuwa akitumika mara chache msimu huu kutokana na majeraha lakini penalti yake aliyofunga katika ushindi wa Chelsea wa 5-1 dhidi ya Southampton katika raundi ya tatu ya Kombe la FA lilikuwa ni goli lake la 7 katika mechi 17, na kumuweka nyuma ya Fernando Torres na Juan Mata tu katika orodha ya vinara wa mabao wa klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment