Simon Msuva wa Yanga (kushoto) akimtoka beki wa Prisons wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. |
Tegete aliyerejea katika makali
yake na kufunga karibu katika kila mechi anayopangwa tangu Yanga waliporejea nchini kutoka katika kambi yao ya
wiki mbili nchini Uturuki, alifunga goli la utangulizi la timu yake katika
dakika ya tisa tu ya mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa na
kuhudhuriwa na maelfu ya mashabiki.
Winga Simon Msuva aliyeng’ara na
kuonekana kuwa nyota wa mchezo alikimbia na mpira katika upande wa kulia wa
uwanja na kupiga krosi ‘kali’ iliyounganishwa moja kwa moja na Tegete na kuwa
miongoni mwa magoli bora kuwahi kufungwa na ‘Wanajangwani’ msimu huu.
Dakika tano baadaye, Elias Maguri
aliisawazishia Prisons 14 baada ya kuwachambua mabeki wa Yanga ‘kama karanga’
na kuingia ndani ya boksi ambapo pia alimlamba chenga kipa Ali Mustafa
‘Barthez’ kabla ya kuukwamisha mpira wavuni kirahisi kwa kupiga shuti jepesi
kuelekea katika lango lililokuwa tupu.
Maafande waliendelea kucheza
‘jihadi’ na kukaribia kupata goli la utangulizi wakati Jeremiah Juma alipobaki
yeye na kipa katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza baada ya kupenyezewa
pasi safi ya ‘goli’ na Nurdin Siha lakini akashikwa kigugumizi na mwishowe
Barthez akauwahi mpira kutoka miguuni mwake. Hadi mapumziko, matokeo yalikuwa
sare ya 1-1.
Prisons walikianza kipindi cha
pili kwa kasi zaidi na kulishambulia mfululizo lango la Yanga kiasi cha kuzima
shangwe za mashabiki wa ‘Wanajangwani’ waliofunika jukwaa kwa fulana za kijani
na njano huku mahasimu wao wa jadi, Simba wakishangilia pasi kali za ‘maafande’
hao wa Mbeya.
Hata hivyo, wenyeji walizinduka
na kurejesha furaha kwa mashabiki wao baada ya kupata goli la pili katika
dakika ya 57 lililofungwa na Mbuyu Twite kufuatia mpira wa kona ‘kali’
iliyopigwa na Niyonzima kuuanganishwa vyema na Msuva kabla ya kutemwa na kipa
Abdallah na kumkuta beki huyo wa kimataifa wa Rwanda aliyeukwamisha wavuni kwa
shuti kali la karibu na lango.
Baada ya bao hilo, Yanga
waliendelea kucheza gonga safi zilizoonyesha matunda ya maandalizi yao ya wiki
mbili nchini Uturuki ambapo katika dakika ya 64, ‘muvu’ iliyomaliziwa kwa krosi
ya Nurdin Bakari ilimkuta Tegete katika nafasi nzuri na bila kufanya makosa,
mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars) akafunga kwa
kuudokolea mpira wavuni.
Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernst
Brandts aliwasifu wapinzani wao na kueleza kuwa amefurahishwa na kiwango
kilichoonyeshwa na timu yake, hasa katika kipindi cha pili.
Kocha Jumanne Chale wa Prisons
alisema kuwa timu yake ilipoteza mechi hiyo kutokana na sababhu za kiufundi,
hasa kwa kumkosa mshambuliaji wao Emmanuel Gabriel aliyeondolewa kikosini muda
mfupi kabla ya mechi baada ya kibali chake kukosekana.
Ushindi wa leo umeifanya Yanga izidi
kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 32, tano
zaidi ya Azam wanaokamata nafasi ya pili baada ya kushinda 3-1 dhidi ya Kagera
Sugar jana na sita zaidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba ambao wamebaki katika
nafasi ya tatu licha ya kuibuka na ushindi wa 3-1 pia dhidi ya African Lyon
jana.
VIKOSI
Yanga: Ali Mustafa ‘Barthez’,
Mbutu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athumani
Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Nurdin Bakari/David Luhende (dk.59), Didier
Kavumbagu/Hamis Kiiza (dk.54), Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Prisons: David Abdallah, Aziz
Sibo, Henry Mwalugala, Jumanne Fadili, Nurdin Issa, Sino Augustino, Fredy
Chudu, Elias Maguri/Julisu Kwanga (74), Misango Magai/John Matei (58) na
Jeremiah Juma.
No comments:
Post a Comment