Saturday, January 26, 2013
GERVINHO, YAYA TOURE WAIPELEKA IVORY COAST HATUA YA MTOANO... ADEBAYOR AFUFUA MATUMAINI YA TOGO
IVORY Coast imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya mtoano ya michuano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuisambaratisha Tunisia kwa magoli 3-0 katika mechi yao ya Kundi D iliyomalizika punde nchini Afrika Kusini.
Winga wa Arsenal, Gervais Kouassi a.k.a Gervinho aliipatia Ivory Coast goli la kuongoza kwa shuti lililotinga kwenye dari baada ya kugongeana na straika wa Anzhi Mckhachkala, Lacina Traore, ambaye alimrejeshea mpira kwa pasi ya kisigino katika dakika ya 21.
Mwanasoka Bora wa Afrika, Yaya Toure, alithibitisha sifa yake barani hapa baada ya kufunga goli kali la pili kwa shuti la kutokea nje ya boksi lililoenda kutinga kwenye nyavu ndogo katika dakika ya 85, kabla ya Didier Yakonan kuhitimisha ushindi mnono wa kujiamini katika dakika ya 88.
Ushindi unamaanisha kwamba Ivory Coast imetinga katika hatua ya mtoano baada ya kufikisha pointi sita. Ivory Coast imefunga magoli matano na kufungwa goli moja.
Katika mechi ya pili ya kundi hilo, Togo iliimarisha nafasi yao ya kusonga mbele baada ya kuifunga Algeria kwa magoli 2-0 na kuwa na pointi tatu sawa na Tunisia.
Straika wa Tottenham ya England, Emmanuel Adebayor aliifungia Togo goli la kuongoza kabla ya mtokea benchi Dome Wome kuipatia timu hiyo goli la pili katika dakika ya pili ya majeruhi.
Katika dakika ya 86, mechi hiyo ilisimama kwa takribani dakika 10 baada ya nguzo ya lango kulegea na kulalia upande mmoja wakati kiungo wa Algeria, Adlene Guedioura, alipotumia nyavu za lango hilo kama breki yake pale alipoingia kwa kasi wavuni katia harakati za kujaribu kufunga golini mwa Togo.
Lango hilo zima lililazimika kung'olewa na kukarabatiwa kabla ya kurejeshwa na mechi ikaendelea kuchezwa kwa takriban dakika nne kabla ya mwamuzi wa akiba kufanya jambo ambalo halikutarajiwa pale alipoinua ubao wa dakika za majeruhi na kuonyesha kuwa zimeongezwa dakika 13.
Muda huo mwingi mno ulizua maswali kwa kuwa hapakuwa na upotezaji wa muda mwingi katika kipindi cha pili. Matokeo hayo yanamaanisha kwamba Algeria wamekuwa ndiyo timu ya kwanza kuaga mashindano hayo.
Cape Verde itacheza dhidi ya Angola kesho Jumapili wakati wenyeji Afrika Kusini watawakaribisha Morocco katika mechi ambazo zitaanza kwa wakati mmoja saa 2:00 usiku.
Afrika Kusini inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne ikifuatwa na Cape Verde na Morocco zenye pointi mbili kila mmoja huku Angola ikiwa mkiani na pointi moja.
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment