Thursday, January 24, 2013

HAZARD AOMBA RADHI KUMPIGA TEKE MUOKOTA-MIPIRA

Hazard akiinama kusikilizia hatma yake baada ya kumpiga teke muokota mipira aliyelala chini
Refa Chris Foy akimtoa Hazard kwa kadi nyekundu
Hazard akisindikizwa nje ya uwanja baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu

KIUNGO wa Chelsea, Eden Hazard ameomba radhi kwa kumpiga teke kijana muokota-mipira wakati wa mechi yao waliyotolewa kwenye kwenye Kombe la Ligi ugenini dhidi ya Swansea.

Mbelgiji huyo alikuwa akijaribu kuchukua mpira kutoka kijana huyo aliyekuwa ameulalia kwa juu.

Hazard, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu ya  moja kwa moja na refa Chris Foy kwa kitendo hicho, baadaye aliiambia Chelsea TV: "Kijana aliweka mwili wake wote juu ya mpira na mimi nilikuwa najaribu kuupiga mpira.

"Nadhani nilipiga mpira na si mvulana. Naomba radhi."

Polisi wa Wales Kusini walisema watachunguza tukio hilo, ambalo lilitokea wakati mpira ulipotoka kwa ajili ya kupigwa "goal kick" katika dakika ya 80.

Meneja wa habari wa Swansea City, Jonathan Wilshere alisema: "Polisi wamemhoji kijana, ambaye jina lake halitajwi kwa sababu umri wake ni chini ya miaka 18.

"Yeye na baba yake walizungumza na polisi na hawafungui mashitaka.

"Alikuwa kwenye chumba cha kuvalia cha Chelsea na alipeana mikono na Hazard. John Terry na Frank Lampard walimkaribisha vyema kwenye chumba cha kuvalia cha Chelsea."

Kocha wa Chelsea, Rafael Benitez alisema wote wawili, mchezaji na kijana waliombana radhi baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Liberty.

Aliongeza: "Wote wamebaini walikuwa na makosa.

"Mvulana aliomba radhi kwa kupoteza muda. Hazard alikuwa amefadhaika na akawa anajaribu kuupata mpira. Aliupiga mpira na akaupata.

"Tunaweza kulichunguza tukio kwa nusu saa lakini sote tunajua kwamba wote walikuwa na makosa.

"Tunalishughulikia ndani, hicho ndicho ninachoweza kusema."

Chelsea na Swansea walitoka sare ya 0-0, na Swansea wakatinga fainali kwa ushindi wa jumla ya magoli 2-0.

Chelsea walihitaji ushindi wa 2-0 ili kuipeleka mechi hiyo katika dakika 30 za nyongeza, lakini hawakuweza kupata hata goli moja nchini Wales.

Nahodha wa Swansea, Ashley Williams alisema baada ya mechi hiyo: "Demba Ba aliniambia kwamba mvulana alikuwa ameushikilia mpira. Nilimuona [Hazard] akimpiga teke kwenye mbavu, huwezi kufanya jambo kama lile."

Kocha wa Swansea, Michael Laudrup alisema: "Nadhani [Hazard] atajutia kitendo chake atakapokiona tena kwenye TV. Mvulana alipaswa kuuachia mpira lakini alisukumwa kisha akapigwa teke.

"Naelewa mchezaji mnapokuwa mmetanguliwa na mko katika presha wakati mwingine unasema ama kufanya mambo ambayo hukupaswa kuyasema ama kuyatenda."

Refa wa zamani wa Ligi Kuu ya England, Dermot Gallagher aliiambia BBC Radio 5 live: "Kulikuwa na adhabu wakati beki wa Liverpool, Jamie Carragher alipotolewa kwa kadi nyekundu baada ya kurusha sarafu kuelekea kwa mashabiki dhidi ya Arsenal kwenye Uwanja wa Highbury mwaka 2002.

"Refa Chris Foy alikuwa sahihi kabisa kumtoa Eden Hazard, ni tukio lisilokubalika. Alikuwa sahihi kabisa kumtoa. Ataripoti suala hilo kwa chama cha soka (FA)."

No comments:

Post a Comment