Henry aliporejea Arsenal |
Henry akiwa katika uzi wa klabu yake ya New York Red Bulls |
KOCHA Arsene Wenger amefuta uwezekano wa mshambuliaji wao wa zamani Thierry Henry kurejea kwa mara ya tatu klabuni Arsenal.
Veterani huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akifanya mazoezi na Gunners kwa ajili ya kujiweka fiti kufuatia kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ya Marekani akiwa na klabu yake ya New York Red Bulls.
Henry alirejea kwa mkopo mwaka jana, akaichezea timu hiyo mechi nne na kuongeza rekodi yake ya muda wote ya kuifungia klabu hiyo kufikia magoli 228. Aliichezea Arsenal jumla ya mechi 377.
Wenger alisema: "Hayuko tayari, amerejea tu akitokea mapumzikoni. Kwa sasa hatuna mpango huo."
Baada ya sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Southampton jana, kocha huyo wa Arsenal alisema kuhusu Henry: "Nadhani ataenda mahala kwingine."
Alipotakiwa afafanue, alisema: "Hapana (haitatokea)."
Henry alirejea Arsenal mwaka 2011 na kufunga goli pekee la mechi katika ushindi wa Gunners wa 1-0 katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Leeds, ikiwa ni dakika 10 tu tangu aingie uwanjani kwa mara ya kwanza na klabu hiyo tangu mwaka 2007.
Mfaransa huyo alifunga pia goli la ushindi la dakika za majeruhi dhidi ya Sunderland katika mechi yake ya kuaga kabla ya kurejea kwenye klabu yake ya MLS, ambako amefunga magoli 15 katika mechi 25 msimu wa mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment