Tuesday, January 15, 2013

RONALDO KUMALIZIA MKATABA WAKE REAL MADRID

Ronaldo akiwa na mpenzi wake Iryna kwenye tuzo za Ballon d'Or

Ronaldo akifurahia kufunga 'hat-trick' dhidi ya Real Sociadad katika mechi ya Kombe la Mfalme kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania Januari 9, 2013.

Ronaldo akifurahia kufunga 'hat-trick' dhidi ya Real Sociadad katika mechi ya Kombe la Mfalme kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania Januari 9, 2013.

CRISTIANO Ronaldo amesema anataka kubaki Real Madrid hadi mkataba wake utakapomalizika, lakini amekiri kwamba hana hakika nini kitatokea baada ya hapo.

Mkataba wa sasa wa straika huyo wa zamani wa Manchester United klabuni Bernabeu unamalizika 2015, lakini amekuwa akihusishwa na mipango ya kuwahama miamba hao wa Hispania.

"Nataka kumaliza mkataba wangu Real Madrid - niko wazi kuhusu hilo," nyota huyo (27) aliiambia tovuti ya FIFA. 

"Baada ya hapo, sawa, sijui nini kitatokea baadaye."

Akizungumza katika mahojiano wakati wa tuzo za Ballon d'Or ambayo yamechapishwa kwenye tovuti rasmi ya FIFA jana, Ronaldo alibainisha kwamba mipango yake ni kukaa Real Madrid kwa angalau miaka miwili.

Imekuja baada ya kudai Septemba mwaka jana kwamba hana furaha katika klabu hiyo bingwa ya Hispania.

Straika huyo Mreno alijiunga na Madrid mwaka 2009 kwa ada ya uhamisho iliyoweka rekodi ya paundi milioni 80 akitokea Manchester United.

Ronaldo atakabiliana kwa mara ya kwanza na klabu yake ya zamani wakati Madrid watakapocheza dhidi ya Man United katika hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Februari.

Huku kikosi cha Jose Mourinho kikiwa kimeachwa kwa pointi 18 na vinara wa La Liga, Barcelona, lengo lao kuu sasa ni kutwaa ubingwa wa Ulaya.

"Kila Madridista anataka ubingwa wa 10 wa Ulaya - tunafahamu sana kuhusu hilo," Ronaldo alisema.

"Haitakuwa rahisi na najua itakuwa ni 50-50, lakini bado najiamini.

"Manchester United wameanza mbio za ubingwa vizuri sana wakati sisi tuko nyuma sana ya wengine, lakini bado, kama tutacheza kwa uwezo tulionao, tunaweza kuwatoa." 


Rekodi za Ronaldo Real Madrid


  • Jumla ya mechi alizocheza: 172
  • Jumla ya magoli aliyofunga: 175
  • Mechi alizocheza msimu huu (2012-13) kwenye La Liga: 18
  • Magoli aliyofunga msimu huu (2012-13) kwenye La Liga: 16

No comments:

Post a Comment