Friday, January 4, 2013

DEMBA BA: UNAPOTAKIWA NA MABINGWA ULAYA, MAAMUZI YANAKUWA NI RAHISI

Demba Ba akishikilia jezi ya Chelsea wakati akitambulishwa kujiunga nayo
Demba Ba (kulia) akishikilia jezi ya klabu yake mpya ya Chelsea pamoja na kocha Rafa Benitez

CHELSEA imemsajili straika Demba Ba kutoka Newcastle kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu kwa ada ya uhamisho ambayo haitajwi.

Inaaminikwa kwamba mkataba wa Ba na Newcastle ulikuwa na kipengele kinachomruhusu kuzungumza na klabu nyingine ikija ofa ya paundi milioni 7.

"Ni raha kuwapo hapa, nina furaha sana na najivunia," straika huyo mwenye umri wa miaka 27 aliiambia tovuti ya klabu ya Chelsea.

"Ilikuwa ni muhimu kwangu, na kwa Newcastle, kumaliza suala la hatma yangu na sasa tunaweza kusonga mbele."

Straika huyo wa Senegal aliongeza: "Hivi sasa wana mwezi mzima wa kusajili mchezaji mwingine. Mimi niko hapa sasa na nahitaji kupazoea.

"Pale klabu iliyoshinda ubingwa wa LIgi ya Klabu Bingwa Ulaya inapokuhitaji, inakuwa ni rahisi sana kufanya maamuzi. Hii ni klabu kubwa na hilo limesaidia katika kufanya maamuzi. Hayakuwa maamuzi magumu."

Ba, ambaye alihamia Newcastle akitokea West Ham Juni 2011, amechukua nafasi ya Daniel Sturridge, ambaye ameondoka Stamford Bridge kwenda kujiunga na Liverpool wiki hii.

Straika huyo mpya atakuwa tayari kucheza mechi ya Kombe la FA kesho dhidi ya Southampton na nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Swansea, lakini hataweza kuichezea Chelsea katika Ligi ya Europa, kwani tayari amecheza michuano hiyo akiwa na Newcastle.

Ba amefunga magoli 13 akiwa na Newcastle msimu huu. Kutua kwake kutasaidia kumpunguzia mzigo straika aliyesajiliwa kwa paundi milioni 50, Fernando Torres.

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 28 amefunga magoli 14 msimu huu, ingawa ni saba tu aliyofunga kwenye ligi.

No comments:

Post a Comment