Straika wa Burkina Faso, Alain Traore (katikati) akishangilia na Jonathan Pitroipa (kulia) wakati wa mechi yao ya Kundi C la fainali za Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini |
Reinford Kalaba (kushoto) akimpa shughuli mchezaji wa Nigeria wakati wa mechi yao ya Kundi C la fainali zaMataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini. Mechi hiyo iliisha kwa sare ya 1-1. |
BURKINA Faso waliobaki 10 uwanjani walikwea kileleni mwa msimamo wa Kundi C la fainali za Mataifa ya Afrika kwa ushindi wa kishindo wa 4-0 dhidi ya Ethiopia.
Burkinabe walipata goli la kuongoza katika kipindi cha kwanza kupitia kwa straika Alain Traore aliyepokea pasi tamu ya juu na kufunga kwa shuti lililotinga kwenye kona ya juu ya lango.
Kipa Abdoulaye Soulama wa Burkina Faso akatolewa kwa kadi nyekundu baada ya kudaka mpira nje ya boksi wakati timu yake ikiongoza kwa goli 1-0.
Kubaki 10 uwanjani kuliifanya Burkina Faso ibadili staili ya kucheza kwa kujaza watu nyuma na kufanya mashambulizi ya kustukiza wakiwatumia wachezaji wao wenye kasi kama Jonathan Pitroipa, kiungo Djakaridja Kone na straika Alain Traore.
Traore akawafungia Burkina Faso goli la pili katika dakika ya 74 kwa shuti kali la nje ya boksi, kabla ya Djakaridja Kone hajawafungia la tatu.
Kiungo mchezesha timu Pitroipa alikamilisha kipigo hicho kikubwa kufuatia shambulizi la kustukiza baada ya Waethiopia kupoteza mpira katikati ya uwanja.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Burkina Faso kushinda mechi katika fainali za Mataifa ya Afrika nje ya ardhi ya nyumbani, ikiwa ni jaribio lao la 22. Mchezaji aliyeingia kutokea benchi Wilfried Balima aliiba mpira huo na kukimbia nao kabla ya kupiga krosi safi iliyomkuta Pitroipa aliyemalizia kiufundi na kuipa Burkina Faso ushindi wa kwanza Mataifa ya Afrika tangu walipofikia hatua ya nusu fainali katika ardhi ya nyumbanui mwaka 1998.
Waethiopia walipata pigo la mapema, baada ya nahodha wao Adane Grima - ambaye aliwafungia goli la kusawazisha liliwapa sare ya 1-1 dhidi ya mabingwa watetezi Zambia katika mechi yao ya ufunguzi - kutolewa kutokana na kupata majeraha ya nyonga.
Matokeo hayo yaliwaweka kileleni mwa msimamo wa Kundi C wakiwa na pointi nne juu ya Nigeria na Zambia, baada ya Super Eagles na Chipolopolo kutoka sare ya 1-1 mapema, na kuisukuma Ethiopia mkiani mwa msimamo wakati wakisubiri matokeo ya mechi zao za raundi ya mwisho.
Nigeria walipata goli kupitia kwa straika Emmanuel Eminike aliyefunga goli lake la pili la michuano lakini mabingwa watetezi Zambia walikuwa na bahati ya kupata penalti ambayo pengine hawakustahili ambayo kipa wao Kennedy Mweene aliifunga kiufundi akiupachika mpira kwenye kona ya juu. Nigeria na Zambia kila moja ina pointi mbili baada ya sare mbili huku Ethiopia ikiwa na pointi moja.
No comments:
Post a Comment