Saturday, January 5, 2013

BOATENG: SIJUI KAMA NITAENDELEA KUCHEZA ITALIA

Kevin-Prince Boateng

Kevin-Prince Boateng

KIUNGO wa AC Milan, Kevin-Prince Boateng amebainisha kwamba huenda akaondoka Italia baada ya kufanyiwa vitendo vya kibaguzi na mashabiki Alhamisi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliondoka kutoka uwanjani baada ya mashabiki kumuimbia nyimbo za kibaguzi wakati wa mechi yao ya kirafiki dhidi ya timu ya daraja la nne ya Pro Patria.

Wachezaji wenzake walimfuata nje ya uwanja na tangu wakati huo amepata sapoti ya timu yake, akiwamo kocha Massimiliano Allegri na rais Silvio Berlusconi, pamoja na watu wakubwa katika ulimwengu wa soka.

Lakini sasa amebainisha kwamba hana hakika na hatma yake katika Serie A.

"Si jambo la kuliacha lipite kiwepesi," aliliambia gazeti la Bild. "Nitalala nalo kwa siku tatu zijazo kisha nitakaa na wakala wangu Roger Wittmann wiki ijayo. Tutakaa na kuangala kama inalipa kuendelea kucheza soka Italia."

Sapoti ya faragha na hadharani ya Berlusconi, ambaye alisema kwamba wachezaji wa timu hiyo wataendelea kutoka nje ya uwanja wakifanyiwa ubaguzi, pamoja na kocha Allegri, huenda visitoshe kumbakisha Boateng nchini humo.

Kiungo huyo wa zamani wa Tottenham aliiambia CNN kwamba anashangaa kwamba ubaguzi bado upo mwaka 2013, na kwamba amechoshwa na kufanyiwa ubaguzi wa namna hiyo.

"Nilishangazwa kwamba katika zama za sasa - mwaka 2013 - mambo haya bado yanatokea; bado tunatakiwa kupambana nayo, na bado tunayasikia," alisema jana Ijumaa.

Aliongeza, "Si mara yangu ya kwanza maishani mwangu kuona mambo kama haya au kusikia mambo kama haya. Nina umri wa miaka 25, na sitaki kusikia upuuzi huu tena, na kwangu mimi, hakuna mtu ambaye atakayeweza kunishawishi nicheze tena. Niliwaeleza moja kwa moja: 'Sitacheza tena kwenye uwanja huu'."

"Nilikuwa nimekasirika, nilifadhaishwa. Na yote haya yalikuja pamoja na nikasema: 'Okay, sitacheza tena. Sitaki kucheza wakati mashabiki wanafanya mambo kama haya, au mahala kama hapa'. Mitazamo hasi mingi ilikuja kwangu.

"Nitamweleza kila mtu kwamba sitaki wacheze katika mazingira kama haya - nitawaeleza watoke uwanjani."

No comments:

Post a Comment