Saturday, December 1, 2012

VITU VYA SHARO MILIONEA VYAPATIKANA... WATUHUMIWA WAKIMBILIA KUISHI MAPORINI KUHOFIA KUKAMATWA

Baadhi ya vitu vya marehemu Sharo Milionea vilivyoibwa baada ya ajali iliyochukua maisha yake. Picha: Issamichuzi.blogspot.com
Baadhi ya vitu vya marehemu Sharo Milionea vilivyoibwa baada ya ajali iliyochukua maisha yake. Picha: Issamichuzi.blogspot.com
MSAKO mkali wa nyumba kwa nyumba uliofanywa kwa ushirikano wa polisi na wananchi umefanikisha kupatikana kwa baadhi ya vitu vya msanii wa filamu na bongofleva marehemu Hussen Mkieti "Sharo Milionea" vilivyoibwa baada ya gari ndogo aliyokuwa akiendesha kupata ajali katika kijiji cha Maguzoni wilayani hapa na kuchukua maisha yake.

Hayo yalisemwa  juzi  usiku na mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu wakati akitokea katika msako huo kwenye kijiji cha Maguzoni ambapo watuhumiwa wamezihama nyumba zao kuhofia kukamatwa.

Mgalu alisema kuwa msako huo wa nguvu uliohusisha jeshi la polisi na wananachi wema wa kijiji cha Maguzoni ulifanyika usiku katika kijiji hicho kwa kupita nyumba hadi nyumba mpaka baadhi ya vitu vya msanii huyo vilipoonekana.

Mkuu huyo wa wilaya alivitaja baadhi ya vitu vilivyopatikana kuwa ni tairi la akiba, radio ya gari, betri ya gari, simu ya mkononi, saa ya mkononi, suruali aina ya jeans na fulana, ambavyo walimvua marehemu na kumuacha na 'boxer' tu.

Mgalu alisema kuwa katika msako huo ambao bado unaendelea, jeshi la polisi liliongozwa na mkuu wa polisi wa wilaya ya Muheza Endrew Satta, mkuu wa upelelezi wilaya aliyefahamika kwa jina la Mgimwa na mkuu wa kituo cha polisi Muheza aliyefahamika kwa jina la Joseph.

Juzi, mkuu huyo wa wilaya alitoa siku mbili vitu hivyo viwe vimeonekana na kama havijaonekana msako mkali wa nyumba kwa nyumba utaingia kijijini hapo wakati alipokuwa akitoa nasaha zake katika mazishi nyumbani kwa msanii huyo Jibandeni kijiji cha Lusanga.

Mbunge wa jimbo la Muheza, Herbert Mntangi, diwani wa viti maalum tarafa ya Ngomeni, Jestina Mntangi, mwenyekiti wa CCM wilaya, Peter Jambele na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Muheza, Amiri Kiroboto wamelaani kitendo hicho na kulitaka jeshi la polisi kufanya kazi yake kuhakikisha vitu vyote vinapatikana

Msanii wa filamu za ucheshi na muziki wa bongofleva, Sharo Milionea, alifariki katika eneo la ajali katika kijiji cha Maguzoni, Muheza wakati gari dogo aina ya Toyota Harrier ilipoacha njia na kupinduka mara kadhaa alipokuwa njiani kwenda kwao Lusanga, Muheza kumuona mama yake akitokea jijini Dar es Salaam.

Sharo Milionea alipata umaarufu mkubwa kupitia staili yake ya kuigiza kama mchekeshaji msafi tofauti na wengi ambao huamini kwamba mchekeshaji ni lazima avae vinyago, kikatuni ama ajipake masizi. Misemo yake ya "kamata mwizi meen", "umebugi meen!" na "ohh mamma!" ilimpa mashabiki wengi hasa watoto.

No comments:

Post a Comment