Saturday, December 1, 2012

NGASSA AFANYA KUFURU, APIGA 5 TANZANIA BARA IKIUA SOMALIA 7-0 NA KUTINGA ROBO FAINALI CHALENJI... YATENGENEZA REKODI YA 7-7-7

Mrisho Ngassa (kulia) akipongezwa na Athuman Idd baada ya kufunga goli la kwanza wakati wa mechi yao ya Kombe la Cecafa Challenge kwenye Uwanja wa Lugogo nchini Uganda leo. Tanzania Bara ilishinda 7-0.
Mrisho Ngasa wa Kilimanjaro Stars (kulia) akipiga shuti mbele ua mabeki wa timu ya Somalia wakati wa mechi yao ya Kombe la Cecafa Challenge kwenye Uwanja wa Lugogo nchini Uganda leo. Tanzania Bara ilishinda 7-0.
Wachezaji wa Kilimanjaro Stars wakisalimiana na wachezaji wa Somalia kabla ya wakati wa mechi yao ya Kombe la Cecafa Challenge kwenye Uwanja wa Lugogo nchini Uganda leo. Tanzania Bara ilishinda 7-0.

MRISHO Ngassa alifunga magoli matano peke yake na John Bocco 'Adebayor' akaongeza mengine mawili wakati timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilipotoa kipigo kikubwa zaidi cha michuano ya Kombe la Chalenji la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa mwaka huu cha magoli 7-0 dhidi ya Somalia katika mechi yao ya mwisho ya Kundi B kwenye Uwanja wa Lugogo, Kampala Uganda leo.

Kipigo cha 7-0 leo, kinarejea matokeo ya 7-0 ambayo Tanzania Bara iliifunga Somalia miaka 7 iliyopita (Desemba 2005) katika michuano hiyo.

Pamoja na kulipa kisasi baada ya Tanzania kufungwa na Somalia 1-0 mwaka jana, ushindi wa leo pia umeipeleka Kili Stars katika robo fainali ya Kombe la Chalenji ikiwa na pointi 6 katika nafasi ya pili ya Kundi B.

Burundi wamemaliza wakiwa vinara wa kundi hilo baada ya kushinda mechi yao ya tatu leo dhidi ya Sudan na kumaliza wakiwa na pointi 9.

Sudan ni wa tatu wakiwa na pointi 3 na watasubiri kuona kama wanaweza kusonga mbele kama 'Best Loosers', lakini Somalia ambao hawajaambulia hata pointi moja watafungasha virago kurejea makwao.

Magoli matano ya leo yanamfanya Ngassa kuwa kinara wa ufungaji katika michuano ya mwaka huu, akifuatiwa na Bocco, ambaye ana ma goli manne baada ya kufunga mawili pia katika mechi ya ufunguzi ambayo Kili Stars walishinda 2-0. 
 

Ngassa alionekana kusahau kwamba anapaswa kuondoka na mpira kwa kufunga 'hat-trick' na alitumia muda wa baada ya firimbi ya mwisho kusalimia mashabiki wachache wa Tanzania waliokuwa pembeni ya uwanja kabla ya refa kumfuata na kumkabidhi mpira wake. 

 Zanzibar Heroes, Kenya, wenyeji Uganda wote pia wameshatinga hatua ya 8-Bora.

No comments:

Post a Comment