Saturday, December 1, 2012
NIYONZIMA AISHANGAA CECAFA SOKA KUCHEZWA KWENYE "SHAMBA LA MPUNGA"
WAKATI kocha wa timu ya soka ya taifa ya Rwanda (Amavubi), Mserbia Sredojevic Milutin 'Micho', amesema bado hawajakata tamaa ya kufika fainali ya Kombe la Chalenji licha ya juzi kukubali kichapo cha magoli 2-1 kutoka kwa Zanzibar Heroes, nahodha Haruna Niyomzima ameshangaa kuona mechi zikiendelea kuchezwa kwenye uwanja uliojaa maji.
Niyonzima alisema anashangazwa kuona CECAFA inaruhusu mechi ziendelee kuchezwa kwenye uwanja ambao haukuwa na sifa.
"Ule haukuwa uwanja wa kuchezea mpira, nashangaa hata kwa nini Rais wao wa nchi (Yoweri Museveni) amekubali mechi ziendelee, najua kwetu (Rwanda) isingekuwa hivi," alisema Niyonzima.
Akizungumza baada ya kupoteza mechi hiyo juzi, Micho, alisema kwamba licha ya kufungwa lakini wachezaji wake walipambana na kulishambulia lango la Zanzibar Heroes bila ya mafanikio.
Micho alisema kwamba baada ya matokeo hayo alipanga kuwapa upya mbinu wachezaji wake ili wafanye vizuri mechi yao ya mwisho dhidi ya Eritrea ambapo anaamini atashinda na kufuzu hatua ya robo fainali.
"Mvua ni moja ya mambo yaliyochangia kuvuruga mipango ya timu zote ingawa tulijua hali hii tangu asubuhi (juzi asubuhi), tutaangalia tulipokosea halafu tunajipanga kwa ajili ya kupata ushindi mechi ya mwisho, bado tunaamini tutafikia malengo yetu," alisema kocha huyo ambaye aliwahi pia kuifundisha Yanga ya Tanzania Bara.
Alisema kwamba baada ya ushindi dhidi ya Malawi, walijipanga lakini hawakuwa na bahati kwa sababu katika soka hali hiyo ipo na ni sehemu ya kujifunza pia.
Niyonzima alieleza pia wapinzani wao Zanzibar Heroes walikuwa na bahati katika mchezo huo kutokana na kipa wao, Mwadini Ally, kufanikiwa kuokoa mashambulizi kadhaa yaliyokuwa yanaelekea kwenye lango lake.
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment