Luis Suarez (kulia) akiifungia Liverpool goli dhidi ya QPR wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Loftus Road mjini London jana Desemba 30, 2012. Liverpool ilishinda 3-0. |
Frank Lampard akishangilia baada ya kuifungia Chelsea dhidi ya Everton wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool jana. Chelsea walishinda 2-1. |
Mashabiki wa Chelsea wakikeba bango la kumuomba mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich usimuache Lampard aondoke wakati wa mechi yao dhidi ya Everton jana. |
KIWANGO kibovu cha QPR kiliiongeza hofu yao ya kushuka daraja wakati walipozamishwa na 3-0 na Liverpool yenye ushawishi mkubwa wa Luis Suarez.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers hakuwapo kwenye mechi hiyo kutokana na kuwa mgonjwa lakini Suarez mara mbili alitumia makosa ya ulinzi na kuwaweka wageni 2-0 ndani ya dakika 16 tu za kwanza.
QPR walinyimwa penalti wakati 'fri-kiki' ya Adel Taarabt ilipougonga mkono wa Jordan Henderson, kabla ya Daniel Agger kuifungia Liverpool goli la tatu kwa kichwa.
Shuti la Steven Gerrard liliokolewa juu ya mstari wa goli la QPR katika mechi ambayo Liverpool walishinda kirahisi.
QPR wanaoshikilia mkia baada ya vipigo 12 katika mechi 20 msimu huu wako hatarini kushuka daraja huku tofauti ya pointi nane ikiwatenganisha na walio katika nafasi ya kunusurika.
Waliwashuhudia wenzao walio pamoja katika nafasi tatu za chini Reading wakishinda na Southampton wakitoka sare Jumamosi na, wakati QPR walitarajiwa kuonyesha nia ya kutaka kubaki katika ligi kuu, jambo hilo halikuwapo.
Liverpool walikuwa na haraka, wenye njaa na ngangari zaidi, na ingawa waliachiwa nafasi ya kutawala mchezo, waliutawala kwa soka la kuvutia ambalo bila ya shaka litamsaidia Rodgers kupona haraka.
Katika mechi iliyochezwa mapema jana Frank Lampard alikumbushia uwezo wake wa kufunga magoli wakati mabao yake mawili yalipoirejesha Chelsea katika nafasi ya tatu ya msimamo kwa ushindi mgumu wa 2-1 dhidi ya Everton.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, alifunga kwa kichwa krosi ya Ramires na akafunga kutokea jirani ya lango baada ya timu yake kuruhusu goli la kutanguliwa katika sekunde ya 62.
Steven Pienaar aliwafungia Everton goli la kuongoza la mapema, baada ya mpira wa kichwa wa Victor Anichebe kugonga nguzo na kumkuta mfungaji.
Nikica Jelavic naye kisha aligongesha nguzo ambayo ingeweza kuwafanya Everton waongoze 2-0 na akaja akakosa nafasi ya wazi ya kuisawazishia timu yake katika dakika za lala-salama.
Ushindi wa nne mfululizo wa Chelsea katika ligi chini ya kocha wa muda Rafael Benitez, baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi zake tatu za kwanza, unamaanisha kwamba Blues wamemaliza mwaka 2012 wakiwa pointi nne nyuma ya Manchester City na 11 nyuma ya Manchester United, lakini wana mechi moja mkononi.
Swali kama Lampard ataongezwa mkataba Stamford Bridge bado ni gumu, huku Muingereza huyo akiwa huru kuzungumza na klabu aitakayo Januari.
Licha ya vipaji vya nyota wapya kama Oscar na Eden Hazard na uwezo usio na shaka wa Juan Mata, mashabiki waliosafiri na timu wa Chelsea waliweka wazi kwamba bado ni mapema sana kumfanya Lampard, ambaye alijiunga na klabu hiyo miaka 11 na nusu iliyopita, awe historia ya timu.
Magoli yake yalihitimisha mwendo mzuri wa Everton bila kufungwa katika mechi 14 kwenye Uwanja wa Goodison Park, tangu walipofungwa kwa mara ya mwisho 1-0 na Arsenal mwezi Machi.
MSIMAMO WA MWISHO WA LIGI KUU YA ENGLAND MWAKA 2012
Nafasi | Timu | Mechi | Goal Difference | Pointi |
---|---|---|---|---|
1. | Man Utd | 20 | 22 | 49 |
2. | Man City | 20 | 19 | 42 |
3. | Chelsea | 19 | 21 | 38 |
4. | Tottenham | 20 | 10 | 36 |
5. | Arsenal | 19 | 18 | 33 |
6. | Everton | 20 | 8 | 33 |
7. | West Brom | 20 | 3 | 33 |
8. | Stoke | 20 | 4 | 29 |
9. | Liverpool | 20 | 5 | 28 |
10. | Swansea | 20 | 5 | 28 |
11. | Norwich | 20 | -9 | 25 |
12. | West Ham | 19 | -1 | 23 |
13. | Sunderland | 20 | -5 | 22 |
14. | Fulham | 20 | -6 | 21 |
15. | Newcastle | 20 | -11 | 20 |
16. | Wigan | 20 | -13 | 18 |
17. | Aston Villa | 20 | -24 | 18 |
18. | Southampton | 19 | -11 | 17 |
19. | Reading | 20 | -15 | 13 |
20. | QPR | 20 | -20 | 10 |
No comments:
Post a Comment