Monday, December 31, 2012

BASIHAYA MABINGWA WAPYA DIWANI CUP

Diwani wa kata ya Bunju, Sharif Issa 'Maji Safi' (kushoto) akimkabidhi kombe la ubingwa wa kata hiyo juzi nahodha wa timu ya Basihaya, Akilimali Bashiri. Basihaya waliibuka mabingwa baada ya kuwafunga Bunju A magoli 2-0 katika mchezo uliofanyika juzi Jumapili kwenye Shule ya Msingi Boko.

Diwani wa kata ya Bunju, Sharif Issa 'Maji Safi' akimkabidhi ufunguo wa pikipiki nahodha wa timu ya Basihaya, Akilimali Bashiri. Basihaya waliibuka mabingwa baada ya kuwafunga Bunju A magoli 2-0 katika mchezo uliofanyika juzi Jumapili kwenye Shule ya Msingi Boko.

Wachezaji wa Basihaya wakishangilia ubingwa wa Diwani Cup baada ya kushinda mechi yao ya fainali dhidi ya Bunju A jana.

Wachezaji wa Basihaya wakishangilia ubingwa wa Diwani Cup baada ya kushinda mechi yao ya fainali dhidi ya Bunju A jana.

Raha ya ushindi... shabiki wa Basihaya akishangilia baada ya timu ya Basihaya kuibuka na ushindi


TIMU ya Basihaya jana ilitwaa ubingwa wa mashindano ya Kombe la Diwani wa Kata ya Bunju baada ya kuifunga Bunju A magoli 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mtambani Boko, jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji tegemeo wa Basihaya, Shabani Abeshi ndiye aliyekuwa nyota wa fainali hiyo baada ya kuifungia timu yake magoli yote mawili -- la kwanza akilitupia katika dakika ya 63 na la pili dakika ya 71.

Kutokana na ushindi huo, Basihaya walizawadiwa na mratibu wa mashindano hayo, Diwani wa kata hiyo, Sharifu Issa 'Maji Safi', pikipiki mpya yenye thamani ya Sh. milioni 1.9, jezi seti moja na kikombe chenye thamani ya Sh. 300,000.

Bunju ambao walikuwa wenyeji wao waliondoka na fedha taslimu Sh. 500,000, jezi seti moja, mpira na kombe lenye thamani ya Sh. 100,000 wakati Boko Stars walioshika nafasi ya tatu walipata Sh. 100,000, jezi seti moja na kombe.

Kamati ya mashindano ilimtangaza, Damas Makwaya wa Boko Stars kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo ambaye alifunga magoli saba, zikiwamo 'hat-trick' mbili.

Diwani Maji Safi aliwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kushiriki kikamilifu kwenye mashindano hayo na ameahidi kuendelea kushirikiana nayo katika kuleta maendeleo kwenye eneo hilo.

Alisema kwamba mwakani anaahidi kuboresha zaidi michuano hiyo na anawaomba waendelee kuwaunga wachezaji wao walioteuliwa kwenye kikosi cha timu ya Kata ambacho kitashiriki kwenye michuano ya Kombe la Meya wa Kinondoni hivi karibuni.

Fainali hizo za juzi zilihudhuriwa na Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Kinondoni, Jumanne Mrimi pamoja na madiwani wengine wa wilaya hiyo.

Bendi ya Msondo Ngoma ilikuwapo kutoa burudani kwa mashabiki kabla na baada ya fainali ambapo wananchi walishuhudia bila ya kulipa kiingilio chochote.

No comments:

Post a Comment