Saturday, December 22, 2012

STARS YAWAKALISHA MABINGWA WA AFRIKA ZAMBIA... NGASSA AMFUNIKA KATONGO UWANJA WA TAIFA

Mshambuliaji wa Taifa Stars, Hamis Mcha (katikati) akiwapa shughuli mabeki wa timu ya Zambia wakati wa mechi yao ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Stars imeshinda goli 1-0. Picha: mrokim.blogspot.com

  Mshambuliaji wa Taifa Stars, Hamis Mcha (kulia) akitoa pande katikati ya wachezaji wa Zambia wakati wa mechi yao ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Stars imeshinda goli 1-0. Picha: mrokim.blogspot.com
  Moses Phiri wa Zambia (kulia) akiwania mpira dhidi ya beki wa Taifa Stars, Aggrey Morris (kushoto) wakati wa mechi yao ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Stars imeshinda goli 1-0. Picha: mrokim.blogspot.com


GOLI pekee kutoka kwa Mrisho Ngassa lilitosha kuifanya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) iwanyamazishe mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) katika mechi yao ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Ngassa alifunga goli hilo katika dakika ya 45 akimalizia vyema pasi ya kiungo mwenzake wa klabu ya Simba, Mwinyi Kazimoto.

Mabingwa wa Afrika Chipolopolo walichezesha nyota wao wote isipokuwa Rainford Kalaba ambaye amebaki nchini England anakochezea klabu ya Southampton.

Mwanasoka Bora wa Afrika wa BBC, Christopher Katongo alikuwamo uwanjani, lakini nyota wa Stars walijipanga vyema kudhibiti hatari za aina zote.

Kuelekea dakika za mwisho wa mechi ambapo wageni walitawala zaidi mchezo, Stars ilinusurika mara kadhaa shukrani kwa nguzo ya lango iliyookoa shuti la Chisamba Lungu katika dakika ya 76 na kazi nzuri ya kipa Juma Kaseja aliyepangua shuti la Felix Katongo, ndugu wa Christopher Katongo, kutokea jirani na lango.

Hata hivyo, si Stars peke yao waliopaswa kuishukuru nguzo ya lango na umahiri wa kipa bali hata Wazambia. Mpira wa kichwa wa Shomari Kapombe kufuatia 'fri-kiki' matata ya Khamis Mcha uligonga nguzo ya goli la Zambia wakati kipa Danny Munyao akiwa ameshakubali matokeo katika dakika ya 8.

Kipa Munyao pia aliiokoa Zambia katika matukio kadhaa likiwamo kudaka kiufundi shuti la dakika ya 71 kutoka kwa Simon Msuva, ambaye alishaanza kushangilia akidhani ni bao kufuatia gonga safi baina yake na Kazimoto.

Ngassa alikaribia kufunga goli lake la pili katika dakika ya 57 wakati alipoikimbilia vyema pasi ndefu ya Salum Abubakar 'Sure Boy' kutokea katikati ya uwanja lakini miguu mirefu ya beki wa TP Mazembe anayewaniwa na Arsenal na Reading, Stopilla Sunzu, ilimnyima uhuru winga huyo mwenye kasi na hivyo kushindwa kupiga shuti zuri na kufanya mpira userereke mbele ya lango na kutoka pembeni kidogo ya nguzo goli la Zambia wakati kipa Munyao akiusindikiza kwa macho.

Stars licha ya kuwakosa washambuliaji wake nyota watatu Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea klabu ya TP Mazembe na John Bocco 'Adebayor', ilicheza soka zuri la chini huku wakitawala katika vipindi tofauti eneo la kiungo lililoshikwa na Sure Boy, Kazimoto, Frank Domayo na Amri Kiemba.Kikosi cha Stars kilikuwa;
Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Kevin Yondani/ Nadir Haroub (dk. 87), Frank Domayo, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa/Amir Maftah (dk.83) na Khamis Mcha ‘Vialli’/ Simon Msuva (dk.59).

Zambia:
Danny Munyao, Chintu Kampamba, Hichani Himonde/ Stopilla Sunzu, Chisamba Lungu, James Chamanga, Moses Phiri/ Mukuka Mulenga, Chris Katongo, Felix Katongo, Nathan Sinkala/ Evans Kangwa, Roderick Kabwe, Isaack Chansa/ Francis Kasonde.No comments:

Post a Comment