Thursday, December 13, 2012

REKODI YA MABAO YA LIONEL MESSI YAPINGWA NA FLAMENGO YA BRAZIL... WADAI ZICO ALIPIGA MAGOLI 89 KATIKA MECHI RASMI MWAKA 1979...! HATA HIVYO, MESSI ATUPIA MENGINE MAWILI NA KUFIKISHA GOLI 88 HUKU AKIBAKIZA MECHI 3

Lionel Messi akiitumikia nchi yake ya Argentina
Lionel Messi akishangilia goli mojawapo akiwa na klabu yake ya Barcelona.


Zico akiitumikia nchi yake ya Brazil
Zico akishangilia goli mojawapo akiwa na klabu yake ya Flamengo ya Brazil 
RIO DE JANEIRO, Brazil
KLABU ya Brazili ya Flamengo inajiandaa kupinga rekodi ya mabao ya Lionel Messi kwa mwaka mmoja wa kalenda, ikisema kuwa nahodha wa zamani wa Brazil, Zico alifunga magoli 89 katika mwaka wa kalenda wa 1979.

Hata hivyo, Messi wa klabu ya Barcelona alifunga magoli yake ya 87 na 88 kwa mwaka huu wa kalenda jana wakati akiisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Cordoba katika mechi yao ya Kombe la Mfalme, huku akiwa tayari ameshavunja rekodi ya mabao 85 iliyokuwa ikishikiliwa na Gerd Mueller tangu mwaka 1972.

"Tumesikitishwa. Messi bado hajaifikia rekodi ya Zico," Bruno Lucena, mkuu wa takwimu na utafiti wa klabu ya Flamengo ameliambia gazeti la michezo la kila siku nchini Brazili liitwalo Lance, akiongeza kuwa Zico aliifungia Flamengo goli 81 mwaka 1979, na mengine saba akayafunga wakati akiichezea timu ya taifa ya Brazil na jingine dhidi ya Argentina wakati akikichezea kikosi cha Nyota 11 wa Dunia.

Aliongeza kuwa mwaka huo, Zico aliumia na kukosa miezi miwili kati ya Septemba na Novemba.

"Kama angecheza kwa mwaka mzima, Zico angefunga zaidi ya magoli 100," alisema.

Lance alionyesha orodha ya magoli katika kila mechi aliyofunga Zico mwaka 1979. Kwa mujibu wa takwimu hizo, Zico alifunga magoli sita katika mechi moja mara mbili, magoli manne katika mechi moja na pia akapiga "hat-trick' tano.

No comments:

Post a Comment