Thursday, December 13, 2012

DIDA AONGEZWA KIKOSINI STARS


TIMU ya Taifa (Taifa Stars) imeingia kambini jana jioni (Desemba 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) huku Kocha Kim Poulsen akimjumuisha tena katika kikosi hicho kipa Deogratias Munishi ‘Dida’.

Kocha Poulsen amemjumuisha tena Munishi kwenye kikosi hicho kuziba nafasi ya Mwadini Ally ambaye atakuwa nje ya nchi na timu yake ya Azam inayokwenda kushiriki mashindano maalumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Wachezaji wote wengine walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wamesharipoti kambini hoteli ya Tansoma, na timu imeanza mazoezi leo asubuhi (Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, na jioni itafanya mazoezi kwenye uwanja huo huo.

Kuanzia kesho jioni (Desemba 14 mwaka huu) itafanya mazoezi Uwanja wa Uwanja wa Taifa wakati mazoezi ya asubuhi yataendelea kuwa Uwanja wa Karume. Wachezaji ambao bado hawajaripoti kambini ni Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira wa kulipwa nchini DRC.

Mechi kati ya Taifa Stars na mabingwa hao wa Afrika itachezwa Desemba 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa. Kocha wa Chipolopolo, Herve Renard ameshataja kikosi chake cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi hiyo.

No comments:

Post a Comment