Inuka sasa....! Pacquiao akimuangalia mpinzani wake Marquez baada ya kumpeleka sakjafuni katika raundi ya tano. |
Chaliiii....! Pacquiao akiwa sakafuni |
Weweeeeee.....! Marquez akishangilia baada ya kumchapa Pacquiao kwa KO usiku wa kuamkia jana.. |
Mmmhh... nimeshinda lakini chamoto nimekiona...! Marquez anavyoonekana usoni baada ya kutandikwa ngumi zaidi ya 90 na Pacquiao usiku wa kuamkia jana Desemba 8, 2012. |
Pambano linalofukuziwa na Manny
Pacquiao dhidi ya Floyd Mayweather, likiwa na thamani ya takriban dola za
Marekani milioni 200 (Sh. bilioni 300), liliangukia sakafuni mjini Las Vegas wakati
Mfilipino huyo alipopigwa ‘kiajabu’ kwa KO katika raundi ya sita na raia wa Mexico,
Juan Manuel Márquez.
Pacquiao alisema baada ya kumalizika
kwa pambano hilo kuwa hatastaafu lakini kipigo hicho kimempunguzia nguvu promota
wake Bob Arum katika mazungumzo kuhusu mgawo wa pambano wanalolifukuzia kwa udi
na uvumba dhidi ya Mayweather.
Majadiliano kuhusu pambano la Pacquiao
na Mmarekani Mayweather ambaye hajawahi kupigwa yamekwama mara kadhaa katika
kipindi cha miaka mitatu sasa.
Pambano alilopigwa Pacquiao linaweza kuitwa
kuwa “pambano la mwaka” baada ya wababe hao kuchapana vikali kwa namna ya
kusisimua.
Wakiwa wamechuana vikali katika kila
mapambano yao matatu yaliyotangulia, ambayo Pacquiao alishinda mawili kwa
tofauti ya pointi chache na kuzua utata kuwa alibebwa huku jingine likimalizika
kwa sare, wote wawili waliapa kuonyesha kiwango cha juu ili kumaliza ubishi
kati yao. Na kweli, walionyesha kiwango cha juu mno kama wenyewe walivyoahidi.
Pacquiao alipelekwa sakafuni katika raundi
ya tatu lakini baadaye akajibu mapigo kwa kumpeleka chini Márquez katika raundi
ya tano.
Wawili waliendelea kuchapana vikali hadi
katika raundi ya sita wakati Pacquiao alipotwangwa ngumi kali na kuanguka vibaya,
akitanguliza uso juu ya sakafu kabla ya mwili kufuata.
Refa Kenny Bayless, alipunga mikono
hewani kuahsiria mwisho wa pambano hilo wakati Márquez akishangilia na kuibua
shangwe kutoka kwa mashabiki wake ndani ya ukumbi wa MGM.
Pacquiao alibaki sakafuni kwa takriban
dakika mbili kabla wapambe wake hawajamsaidia kusimama.
“Nilirusha ngumi jiwe,” Márquez alisema.
“Nilijua Manny atanipiga kwa KO katika
dakika yoyote ile. Nilifikiri kwamba atanipiga kwa KO katika raundi tatu za
mwisho na nilijua kwamba ataachia nafasi.”
Licha ya ushindi wake, Marquez chamoto
alikiona kwani alipigwa ngumi 94 zilizompata kisawasawa dhidi ya 52 alizorusha
yeye. Márquez pia alishavunjwa mfupa wa pua kabla ya raundi ya sita na muda
wote alikuwa akivuja damu na kupumua kwa shida.
Hadi kufikia raundi ya tano, majaji
wote walikuwa wakimpa Pacquiao ushindi wa pointi 47–46.
“Nimepigwa kwa ngumi ambayo sikuiona,”
alisema Pacquiao baada ya pambano hilo, huku akipepesa macho yake kwa shida.
Kabla ya pambano la usiku wa jana, Pacquiao
ambaye pia ni msanii wa muziki na mwanasiasa maarufu anayeshikilia ubunge
katika jimbo moja nchini kwao (Phillipines), alikuwa hajawahi kupigwa kwa KO tangu
mwaka 1999.
No comments:
Post a Comment