Monday, December 10, 2012

MESSI AVUNJA REKODI YA GERD MULLER, AFIKISHA MABAO 86.... FALCAO NAYE HATARIII, ATUPIA 5 ATLETICO IKISHINDA 6-0

Asante Mungu nimempita Gerd Muller... mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi akishangilia goli lake la 86 msimu huu jana usiku dhidi ya Real Betis.
Messi akishangilia kuvunja rekodi ya mabao 85 iliyowekwa na Mjerumani Gerd Muller mwaka 1972. Messi alifunga mabao mawili dhidi ya Real Betis jana na kufikisha jumla ya mabao 86 mwaka huu 2012. Ana mechi tatu kabla ya kuumaliza mwaka huu.
Falcao wa Atletico Madrid akishangilia moja ya mabao yake matano dhidi ya Deportivo Coruna jana usiku. Atletico walishinda 6-0.
Shujaa wa mabao MATANO, Radamel Falcao wa Atletico Madrid akishangilia moja ya mabao yake dhidi ya Deportivo Coruna jana usiku. Atletico walishinda 6-0.

MADRID, Hispania
LIONEL Messi asiyezuilika ameweka rekodi mpya ya kufunga mabao mengi zaidi kwa mwaka mmoja wa kalenda katika historia ya soka duniani na kuwasaidia vinara ambao hawajapoteza mechi katika La Liga, Barcelona, kuendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi sita juu ya Atletico Madrid kufuatia ushindi mgumu 2-1 ugenini dhidi ya Real Betis jana.

Mwanasoka Bora wa Dunia Messi alifunga goli lake la 85 na la 86 kwa mwaka 2012 katika mechi iliyojaa ushindani kwenye uwanja wa Benito Villamarin mjini Seville na kuipiku rekodi ya mabao 85 iliyowekwa na Mjerumani Gerd Mueller mwaka 1972.

Tukio hilo la kihistoria la Messi lilifunika mambo makubwa yaliyofanywa jana usiku na mshambuliaji Atletico, Radamel Falcao, ambaye mapema alifunga magoli matano peke yake wakati walipoisambaratisha timu inayoburuta mkia ya Deportivo Coruna kwa mabao 6-0 nyumbani.

Mshambuliaji huyo wa Colombia, anayefahamika kama 'the tiger' na ambaye anagombewa na klabu tajiri zaidi za Ulaya, alifikisha jumla ya mabao yake msimu huu kuwa 16 katika mechi 15 wakati Atletico ikidumisha tofauti ya pointi tano juu ya mahasimu wao wa mji mmoja Real Madrid.

Kikosi cha Jose Mourinho cha Real kililazimika kuzinduka kutoka nyuma mara mbili na kupata ushindi mgumu wa 3-2 ugenini dhidi ya Real Valladolid Jumamosi ambao uliwasaidia kupunguza pengo la pointi dhidi ya Atletico, ambao waliwafunga 2-0 wikiendi iliyopita, kuwa pointi mbili kwa usiku huo.

Hata hivyo, Atletico walijibu kwa kushinda mechi yao ya 12 katika 15 za ligi msimu huu dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Depor ambayo iko hatarini kurejea moja kwa moja daraja la pili.

Barca wameshinda mechi zao zote msimu huu ukiacha sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Real Madrid Oktoba na magoli mawili ya Messi yaliwafanya wafikishe pointi 43, huku Atletico wakiwa na pointi 37 na Real wana pointi 32. Betis ni wa tano wakiwa na pointi 25, sawa na wanaoshikilia nafasi ya nne Malaga, ambao waliwasambaratisha Granada 4-0 Jumamosi.

"Inaonekana kama jambo lisilowezekana kwamba yeye (Messi) anaweza kufunga magoli mengi kiasi hiki ndani ya mwaka mmoja lakini kuna mechi tatu zimebaki na tunatumai kwamba ataendelea kuongeza jumla ya mabao yake," kocha wa Barca, Tito Vilanova, aliuambia mkutano na waandishi wa habari.

"Tunatumai kwamba atakwenda mbali sana katika maisha yake ya soka kwa sababu bado ni mdogo sana," aliongeza. "Sidhani kama tutaona mchezaji mwingine kama yeye."

BETIS WASIO NA BAHATI
Kikosi cha Vilanova kiliwatawala Betis kama ilivyotarajiwa katika kipindi lakini wakapoteza umiliki baada ya mapumziko na mwamba wa lango uliinyima timu hiyo goli mara tatu.

Messi aliifikia rekodi ya Mueller wakati alipochukua mpira katika eneo la katikati katika dakika ya 16 na akaiacha safu ya ulinzi ya Betis ikiwa imesimama kabla ya kufunga kwa shuti la pembeni chini kulia.

Pasi ya 'akili' ya kisigino ya Andres Iniesta ilimpikia Messi goli la pili dakika tisa baadaye kwa shuti kali kutokea katika eneo lile lile la kwanza ndani kidogo ya boksi na mpira ukatumbukia kwenye kona ile ile ya lango.

Ruben Castro alirudisha goli moja kwa wenyeji katika dakika ya 39 na kufanya kipindi cha pili kuwa kigumu zaidi kwa wageni.

Messi alikaribia kufunga 'hat-trick' dakika tano kabla ya mechi kumalizika wakati alipopiga 'tikitaka' ya jirani na lango lakini kipa wa Beti, Adrian alipangua mpira huo ambao ulimrudia Jordi Alba ambaye shuti lake liligonga 'besela' na mpira kutoka nje.

Kipigo kilikuwa kigumu kwa Betis, ambao waliwachapa Real 1-0 nyumbani mwezi uliopita na kuwapa Barca moja ya mitihani migumu zaidi kufikia sasa msimu huu ambao ulistahili japo pointi moja.

Mshambuliaji wa Atletico, Diego Costa alirekebisha makosa ya kadi nyekundu aliyopewa Alhamisi kwenye Ligi ya Europa wakati alipofunga goli la kuongeza kwenye Uwanja wa Calderon kwa kichwa kutokana na kona iliyopigwa na Koke katika dakika ya 23.

Kiungo wa Depor, Juan Valeron alipiga kichwa kilichogonga nguzo dakika nne baadaye lakini Atletico waliongeza la pili wakati Falcao alipoikimbilia vyema pasi ya Koke na kufumua shuti la chini lililotinga kwenye kona ya wavu.

Mpira uliorushwa haraka kutokea kushoto dakika tatu kabla ya mapumziko ulimpikia goli la pili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 na akafumua shuti kali lililomshinda kipa Daniel Aranzubia kutokea kwenye kona ya eneo la penalti.

Falcao kisha akaangushwa ndani ya boksi na akafunga penalti hiyo katika dakika ya 64 na kukamilisha 'hat-trick' yake, akafunga kwa kichwa la nne na akakamilisha lake la tano katika dakika ya 71.

Yeye ni mchezaji wa kwanza kufunga magoli matano katika mechi ya La Liga tangu Fernando Morientes alipofanya hivyo kwa Real Madrid dhidi ya Las Palmas mwaka 2002.

MALLORCA AIBU
Real Mallorca waliendelea kuporomoka kuelekea kushuka daraja wakati walipofungwa 4-0 ugenini Levante, kikiwa ni kipigo cha nane katika mechi 10 walizocheza bila ya ushindi.

Obafemi Martins aliwafungia Levante goli la kuongoza kabla ya mapumziko na David Navarro, Ruben Garcia na Vicente Iborra walifunga katika kipindi cha dakika 10 katika kipindi cha pili.

Levante, ambao wamefuzu hatua ya 32-Bora ya Ligi ya Europa, wako katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 24, huku Mallorca wakiwa katika nafasi ya 17 kwa pointi 13.

Timu inayochechemea ya Athletic Bilbao ilipata ushindi wa tano tu msimu huu wakati waliposhinda 1-0 nyumbani dhidi ya Celta Vigo.

Goli la kichwa la Aritz Aduriz katika dakika ya 33 liliamua mechi kwenye uwanja wa San Mames na kuiinua Bilbao hadi nafasi ya  13 wakiwa na pointi 18 points. Celta wako katika nafasi ya 15 kwa pointi 15.

No comments:

Post a Comment