Sunday, December 23, 2012

MOURINHO: SIJIUZULU, SIHOFII KIBARUA CHANGU

Jose Mourinho akishuhudia mechi yao ya kipigo cha 3-2  jana usiku.

Tunahujumiana... Ronaldo (katikati) akishika kiuno baada ya kufungwa jana usiku. Kushoto ni Ozil na kulia Benzema

Tumerogwa?..... Xabi Alonso (kushoto) akijiuliza baada ya Real Madrid kufungwa goli jingine huku wachezaji wa Malaga wakishangilia jana usiku

KOCHA Jose Mourinho amesisitiza kwamba hatajiuzulu kuifundisha Real Madrid baada ya timu yake kukumbana na kipigo cha 3-2 jana usiku na kuanguka pointi 16 nyuma ya vinara Barcelona.

Mourinho alionekana kutokubali ukweli wakati alipoulizwa kama anahofia ajira yake.

"Sihofii kabisa na wala sitajiuzulu," alisema. "Mimi si mtoto, najua kwamba matokeo ndiyo kila kitu.

"Kama unaona kwamba wachezaji hawataki kuendelea mimi nakuwa muwazi kabisa. Lakini haiko hivyo. Tulichokosa ni bahati tu."

Isco aliwafungia Malaga goli la kuongoza katika dakika ya 49 kabla ya goli la kujifunga kutoka kwa Samuel Sanchez kuisawazishia Real. Mshambuliaji wa zamani wa Blackburn na Manchester City, Roque Santa Cruz aliipa Malaga magoli mawili ya haraka wakati alipofunga katika dakika 73 na ya 76 baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba.

Karim Benzema akapunguza moja zikiwa zimebaki dakika nane, lakini walikuwa tayari wamechelewa sana kuizuia Malaga isipate ushindi wao wa kwanza dhidi ya Real tangu mwaka 1983.

Mourinho alikiri kwamba uwezekano wa Real kutetea ubingwa wao sasa umekwisha.

"Nadhani ni uongozi mkubwa mno usiokamatika. Msimu uliopita tulitwaa ubingwa kwa tofauti kama hiyo lakini sasa hatuendi vyema. Sina furaha na kilichotokea lakini huu ndiyo ukweli," alisema.

Mreno huyo pia alitetea maamuzi yake ya kumtupa benchi kipa Iker Casillas, na kumuanzisha Antonio Adan (25).

Ilikuwa ni mara ya kwanza katika miaka 10 kwa kipa huyo mshindi wa Kombe la Dunia kuachwa nje ya kikosi cha Real.

"Kwa sasa, kwangu na benchi langu la ufundi, Adan ni bora zaidi ya Iker," Mourinho alisema. "Tumekuwa tukichechemea katika maeneo mengi, mojawapo ni ulinzi. Kocha ndiye anayechanganua ni nani aliye katika hali bora ya kucheza na anachagua timu yake na hicho ndicho nilichokifanya.

"Nyie [vyombo vya habari] mnaweza kutafsiri mpendavyo lakini ni maamuzi ya kiufundi tu."

No comments:

Post a Comment