Tuesday, December 4, 2012

MOURINHO ATOA MPYA... AJITOKEZA UWANJANI DAKIKA 40 KABLA MECHI YA KLABU YAKE REAL MADRID DHIDI YA ATLETICO MADRID ILI MASHABIKI WASIOMTAKA WAPATE NAFASI YA KUMZOMEA KADRI WATAKAVYO LAKINI AKIWASIHI KUWASHANGILIA WACHEZAJI WAKE MWANZO-MWISHO... HATA HIVYO, ALIPOJITOKEZA TU UWANJA UKALIPUKA KWA KUMSHANGILIA NA KUMSIFU KWA KUTAJA JINA LAKE... MWISHOWE REAL WAKASHINDA 2-0 DHIDI YA KINA FALCAO!

Baadhi ya mashabiki wa Real Madrid wakiinua mabango yenye ujumbe mbalimba wa kumuunga mkono kocha Jose Mourinho kabla ya kuanza kwa mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Atletico Madrid kwenye Uwnanja wa Santiago Bernabeu juzi Jumamosi Desemba 1, 2012. Real walishinda 2-0. 
MADRID, Hispania
Kocha José Mourinho wa Real Madrid alitoa kali ya mwaka kabla ya mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya mahasimu wao wa jad, Atletico Madrid Jumamosi baada ya kutimiza ahadi yake ya kujitokeza uwanjani dakika 40 kabla ya kuanza kwa mechi ili awape nafasi mashabiki wasiomtaka wamzomee na kumwagia mitusi yote watakayo lakini akiwasihi kuwa wasifanye hivyo kwa wachezaji wake ambao alitaka washangiliwe kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho.

Kama alivyokuwa ameahidi siku moja kabla ya mechi, Mourinho alijitokeza kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu saa 3:20 usiku na kusimama pembeni ya mstari wa Uwanja huku akiwatazama mashabiki ili wapate nafasi ya kutimiza kiu yao ya kumzomea kadri watakavyo.

Hata hivyo, kusudio la Mourinho la kukata kiu ya mashabiki wanaomchukia lilielekea kugonga mwamba kwani badala ya kuzomewa, mashabiki takriban 3,000 waliokuwa wameshaketi katika viti vyaomida hiyo walimpokea kwa shangwe na vifijo huku wakimtukuza kwa kulitaja jina lake na wengine wakifika uwanjani na mabango yanauyomtaja kuwa yeye "ndiye nambari 1".

Shangwe hizo kubwa kwake zilizima sauti za watu wachache waliokuwa wakipiga miluzi kwa nia ya kumzomea; jambo lililomfanya kocha huyo asione umuhimu wa kuendelea kubaki uwanjani hapo na badala yake, akawasalimia kidogo na kutimka zake.

Baadaye, kikosi cha Mourinho kilishangiliwa pia kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho kama alivyokuwa ameomba kocha huyo na mamabo yakawaendea poa baada ya kutandaza soka safi, wakiwapeleka puta kina Radamel Falcao na Diego Costa waliokuwa wakiusaka mpira kwa tochi katika muda mwingi wa mechi.

Mwishowe, Real Madrid wakaibuka na ushindi wa mabao 2-0, shukrani zikienda kwa Cristiano Ronaldo aliyetangulia kufunga kwa 'fri-kiki' kali kabla baadaye hajatoa pasi iliyozaa goli la pili lililofungwa na Mesut Ozil.

Awali, Mourinho alitangaza mpango wake wa kujitokeza uwanjani mapema akiwa peke yake ili abebe yeye mzigo wa kuzomewa na baadhi ya mashabiki wanaompinga klabuni hapo, na ambao walifanya hivyo kwa kumzomea Jumanne wakati wa mechi yao ya Kombe la Mfalme waliyoshinda 3-0 dhidi ya Alcoyano.

Mourinho alijua mapema kwamba baadhi ya mashabiki hawamkubali na hivyo wangemzomea katika mechi yao dhidi ya Atletico ambao ni mahasimu wao wa jadi katika jiji la Madrid.

Hata hivyo, kocha huyo Mreno alipata ushindi wa kishindo dhidi ya kura ya mashabiki ya kutokuwa na imani naye kwani waliomshangilia na kumsifu kwa kutaja jina lake na kupunga mabango walikuwa wengi kulinganisha na wale waliojaribu kumzomea kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu Jumam
osi.

No comments:

Post a Comment