Monday, December 3, 2012

KILI STARS, Z'BAR HEROES ZATINGA NUSU FAINALI CHALENJI


Na Mwandishi Wetu, Kampala
TANZANIA Bara na Zanzibar Heroes zimetinga nusu-fainali ya Kombe la Chalenji la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati baada ya kushinda mechi zao za robo fainali kwenye Uwanja wa KCC, uliopo Lugogo nchini Uganda leo.

Kilimanjaro Stars ya Bara ilishinda 2-0 dhidi ya Amavubi ya Rwanda, shukrani kwa mabao ya Amri Kiemba na John Bocco, aliyefunga bao lake la tano katika michuano hiyo mwaka huu na kuungana na nyota mwenzake wa Bara, Mrisho Ngassa, kuongoza katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu.

Zanzibar Heroes ilishinda kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 za mechi yao kumalizika kwa sare ya 0-0. Hapakuwa na dakika 30 za nyongeza, utaratibu ambao utaanza kutumika katika hatua ya nusu fainali.

Zanzibar iliwalipia kisasi ndugu zao wa Bara ambao walilala 1-0 mikononi mwa Burundi katika hatua ya makundi, baada ya kipa Mwadini Ali wa Zanzibar kudaka penalti moja ya Abdoul Fiston huku nahodha Selemani Ndikumana akipaisha yake.

Mchezaji pekee wa Zanzibar aliyekosa penalti alikuwa ni beki Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye shuti lake lilidakwa na kipa Ndoli wakati waliofunga penalti zao walikuwa Khamis Mcha, Jaku Juma, Adeyom Abdul, Samih Nuhu, Aggrey Morris na Abdallah Othman.

Mechi nyingine mbili za robo fainali zitachezwa kesho, ambapo Kenya itaikabili Malawi mchana itakayofuatiwa na wenyeji Uganda dhidi ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Mandela.

Tanzania Bara itacheza dhidi ya mshindi wa mechi ya Uganda na Ethiopia, wakati Z'bar iwakutana na mshindi wa mechi baina ya Malawi na Kenya.Mechi zote mbili za nusu fainali zitachezwa Alhamisi.

Hadi mapumziko, Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya 34 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.

Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.

Katika hicho kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19 Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.

Stars pamoja na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha na ikawapita wote.

Ngassa tena, katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda nje sentimita chache.

Kipindi cha pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.

Hata hivyo, walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili 54 baada ya John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.

Baada ya bao hilo, Rwanda walionekana kupagawa, lakini hawakusahau kushambulia lango la Stars na dakika ya 86 Dadi Birori hakujali ameotea akasukuma mpira nyavuni, lakini refa akakataa bao hilo.

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema baada ya mchezo kuwa wachezaji wake walijituma wakati wote uwanjani na ikazaa matunda. “Vijana walikuwa na ari ya kufunga, wakatengeneza nafasi na wakapata magoli mawili ya muhimu,” alisema.

Alisema timu yake ina vijana wengi na mashindano haya yamewapa uzoefu mkubwa kwani wamepambana na timu kubwa na kuzipa wakati mgumu.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, alituma salamu za pongezi kwa Stars huku akisema walistahili kushinda na kuna dalili zote kuwa watacheza fainali Jumamosi Disemba 8.

“Sisi kama wadhamini tunafarajika sana kuona timu inafanya vizuri..tunawatakia kila la heri waendelee hivi hivi na kwenye mashindano mengine ili wazidi kuipeperusha bendera ya Tanzania,” alisema.

Watanzania waishio Kampala na wengine kutoka mkoa wa Kagera walijitokeza kwa wingi na kuishangilia Stars kwa nguvu zote. Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Lodslaus Komba naye alihudhuria mechi hiyo.

Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Amri Kiemba, Salum Abubakar/Athumani Iddi dk51, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa na John Bocco/Shaaban Nditi dk 85.

Rwanda; Jean Claude Ndoli, Emery Basiyenge, Ismail Nshutimayamangara/Fabrice Twagizimana dk19, Jimmy Mbaraga/Imran Nshiyimana dk67, Charles Tibingana/Barnabe Mbuyumbyi dk61, Michel Rusheshangoga, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Jean Claude Iranzi, Dadi Birori na Tumaine Ntamuhanga.

No comments:

Post a Comment