Monday, December 24, 2012

MESSI AFUNGA MWAKA NA REKODI KIBAO

Lionel Messi

LIONEL Messi amemaliza mwaka 2012 kwa kasi ile ile aliyokuwa nayo wakati akiuanza, ya kufunga. Amefunga jumla ya magoli 91, na kuipita kwa magoli 6 rekodi iliyodumu kwa miaka 40 ya magoli 85 iliyowekwa na gwiji wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Gerd 'Torpedo' Muller mwaka 1972.

Pamoja na hiyo, Messi a.k.a 'La Pulga' amekuwa mchezaji wa sita tu wa Barcelona katika historia ya klabu hiyo kufunga katika mechi saba mfululizo. Kufikia sasa, wachezaji pekee waliofanya hivyo ni Martín (mechi 10 mfululizo), Ronaldo (10), Cesar Rodriguez (7), Kubala (7) na Johan Cruyff (7). Messi sasa amejumuika katika orodha hiyo na anaweza kushika nafasi ya tatu miongoni mwao kama atafunga goli dhidi ya Espanyol katika mechi ya mahasimu wa Catalunya Januari 6.

Messi pia anaenda katika mapumziko ya Krismasi akiongoza kirahisi orodha ya wafungaji wa La Liga akiwa na mabao 25. Tayari ameshafunga nusu ya magoli aliyofunga msimu mzima uliopita ilhali ndiyo kwanza kuna mechi mbili bado za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa msimu huu.

La Pulga amemaliza mwaka kwa kuingia katika vitabu vya rekodi ambavyo huenda vikamshuhudia akishinda tuzo ya Ballon d’Or ya mwanasoka bora kwa mwaka wa nne mfululizo. Licha ya kutoshinda taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wala la Ligi Kuu ya Hispania mwaka 2012, magoli yake aliyofunga yanampa nafasi kubwa zaidi ya kubeba tuzo hiyo kwa mara ya nne na kuwapiku magwiji kama Marco Van Basten au Michel Platini.

No comments:

Post a Comment