Tuesday, December 25, 2012

AFUKUZWA KAZI KWA VILE "ANAVUTIA MNO KIMAPENZI"

Melissa Nelson

BAADA ya kufanya kazi ya msaidizi wa tiba ya meno kwa miaka 10, Melissa Nelson amefukuzwa kazi kwa kuwa na "mvuto mno" na tishio kwa ndoa ya mwajiri wake.

"Nadhani si sahihi hata kidogo," Melissa alisema. "Nadhani inatuma ujumbe kwamba wanaume wanaweza kufanya chochote wanachotaka katika ajira."

Ijumaa, Mahakama Kuu ya Mkoa ya Iowa, Marekani iliamua kwamba James Knight, bosi wa Melissa, alikuwa ndani ya haki za kisheria wakati alipomfukuza kazi mwanamke huyo, wakiafiki maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya chini.

"Tunadhani kwamba mahakama ya ilitoa maamuzi sahihi," alisema Stuart Cochrane, wakili wa James Knight. "Msimamo wetu daima ulikuwa ni kwamba Mrs. Nelson hakufukuzwa kazi kwa sababu ya jinsi yake, alifukuzwa kwa sababu tabia yake haikuwa muafaka mahala pa kazi. Ni mwanamke mwenye mvuto sana. Dr. Knight aliona kwamba tabia zake na mavazi hayakuwa muafaka."

Kwa Melissa, mwanamke mwenye umri wa miaka 32 mke wa mtu na mama wa watoto wawili, taarifa za kufukuzwa kazi na sababu zilizotolewa zilikuja kwa mshtuko mkubwa.

"Nilishangazwa baada ya kufanya kazi kwa miaka mingi mno bega kwa bega sikuwa na wazo lolote kwamba niliingia akili mwake," alisema Melissa.

Wawili hao hawajawahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi au kutongozana, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, hata hivyo katika mwaka mmoja na nusu wa mwisho wa ajira ya Melissa, Knight alianza kutoa maoni kuhusu mavazi yake mwanamke huyo kwamba yanabana sana na yanampunguzia umakini.

Miezi sita kabla ya Melissa kufukuzwa, mwanamke huyo na bosi wake walianza kuandikiana meseji kuhusu kazi na mambo binafsi, kama kupeana habari mpya kuhusu watoto wao, mahakama iliambiwa.

Meseji zilikuwa za kawaida, lakini Melissa anakumbuka kupokea moja kutoka kwa bosi wake akimuuliza mwanamke huyo "ni mara ngapi amefurahia 'kufika kileleni'."

Melissa hakuijibu meseji hiyo na wala hakuonyesha kama alikoseshwa amani na swali hilo, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama.

Muda mfupi baadaye, mke wa Knight, Jeanne, ambaye pia anafanya kazi mahala hapo, alibaini kuhusu meseji hizo na akamuamuru mumewe amfukuze Melissa.

Wanandoa hao waliwasiliana na mchungaji mkongwe wa kanisa lao na alikubali kwamba Melissa afukuzwe kazi ili kuokoa ndoa yao, Cochrane alisema.

Januari 4, 2010, Melissa aliitwa kwenye kikao na Knight huku mchungaji huyo akiwapo. Knight akasoma taarifa iliyoandaliwa akimweleza Melissa kwamba amefukuzwa kazi.

"Dr. Knight aliona kwamba kwa manufaa ya ndoa yake na ya mwanamke huyo ni vyema akasitisha ajira yake," Cochrane alisema.

Knight alikiri katika nyaraka za mahakamani kwamba Melissa alikuwa mchapakazi mzuri na kwa sababu hiyo alikuwa akipewa heshima zote.

"Nimefadhaishwa sana. Hakika nimefadhaishwa," alisema Melissa.

Mume wa Melissa alipojaribu kuwasiliana na Knight kujua sababu, daktari huyo wa meno alimweleza keamba "alihofia kwamba angekuja kuingia naye katika mahusiano siku za mbele kama asingemfukuza."

Paige Fiedler, wakili wa Melissa, alisema katika taarifa yake aliyoitoa kwa ABC News akisema amechefuliwa na hukumu hiyo.

"Tumeshangazwa na hukumu ya mahakama na inaonyesha kushindwa kutambua manyanyaso ya jinsia," aliandika.

"Ingawa watu hufanya maamuzi kwa sababu mbalimbali, ni kawaida kwa wanawake kuonewa kiubaguzi kutokana na mvuto wao au kukosa mvuto wa kimapenzi. Huo ni ubaguzi wa kijinsia," Fiedler aliandika. "Takriban kila mwanamke mjini Iowa analifahamu hili kwa sababu tumeshalishuhudia sana."

No comments:

Post a Comment