Monday, December 24, 2012

MASHABIKI REAL MADRID "WAMFUKUZA" MOURINHO... KURA YA MAONI YAPIGWA... ASILIMIA 82 WASEMA AONDOKE

Jose Mourinho

MASHABIKI wa Real Madrid wametoa maamuzi yao. Wanataka Mourinho afukuzwe Bernabeu. Matokeo mabovu katika msimu huu hadi sasa, yanayoambatana na mivutano inayoripotiwa baina ya Mreno huyo na baadhi ya wachezaji na vyombo vya habari, imewachosha, na sasa wamesema "INATOSHA".

Baada ya kumuweka benchi nahodha Iker Casillas katika mechi yao dhidi ya Malaga imekuwa ni moja ya mambo yaliyowachefua mashabiki. Kufuatia utafiti uliofanywa na tovuti ya nchini Hispania  ulioweka swali lililosema "Real Madrid imfukuze Mourinho?" watu takriban 100,000 wa Real walijibu ambapo asilimia 82.4 ilisema "NDIYO".

Inaonekana sasa mapenzi yaliyokuwapo baina ya kocha huyo Mreno na mashabiki wake yamekwisha, na mvunjiko ulionekana katika mechi ya Kombe la Mfalme dhidi ya Alcoyano, ambapo mashabiki wengi wa Real walimzomea na kumpigia miluzi kocha wao, huku wengine wakidiriki hata kuwazomea wenzao waliojaribu kumsapoti Mourinho uwanjani.

Zaidi, jambo hili linaweza kuonekana hata katika mitandao yote mikubwa ya kijamii, ambapo maoni ya kumsapoti yanapotea na kugeuka kuwa shutuma.

Kitendo cha kumtupa benchi mmoja wa magwiji wa Real Madrid - Iker Casillas - inaonekana ni kuanzisha vita dhidi ya mashabiki damu wa Madrid wanaojulikana kama 'Madridistas'.

Mourinho inawezekana kwamba ameamua ama hajaamua kuondoka mwisho wa msimu, lakini lililo wazi ni kwamba hata kama hajaamua 'kuruka nje ya boti', kuna watu wengi sana wanaotaka kuona akitimuliwa.

No comments:

Post a Comment