Wednesday, December 19, 2012

MBUNGE WA ZAMANI TABORA MJINI -- SIRAJU KABOYONGA AFARIKI DUNIA... NI YULE ALIYENG'OLEWA NA RAGE 2010

Marehemu Siraju Kaboyonga enzi za uhai wake.
Mbunge wa zamani wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA), Siraju Juma Kaboyonga, amefariki dunia jijini Dar es Salaam saa 4:00 usiku wa kuamkia leo Desemba 19, 2012.

"Tunasikitika kuwa leo tumeamka tukiwa na majonzi makubwa baada ya kumpoteza mwenyekiti wetu, Siraju Kaboyonga," amesema Sara wakati akiwa katika mahojiano na mtangazaji Godfrey Gondwe wa kituo cha luninga cha ITV leo asubuhi.

Taarifa zaidi kutoka kwa ndugu wa marehemu, Haji Kaboyonga, zimedai kuwa marehemu (Siraju Kaboyonga) alikuwa akisumbuliwa na maradhi na alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. 


Amesema atazikwa jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi (Desemba 20, 2012) saa 7:00 mchana, kwenye makaburi ya Kisutu na shughuli za mazishi zinaendelea nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam.

Enzi za uhai wake wa kuwa mbunge, Kaboyonga alikuwa akionyesha uwezo mkubwa wa masuala ya uchumi, hasa fedha na benki.

Aling'olewa katika nafasi yake ya ubunge wa Tabora Mjini baada ya kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM na mbunge wa sasa wa jimbo hilo na Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage.


Hivi karibuni aligombea pia ubunge wa Afrika Mashariki huku akiomba kura akiwa katika 'wheel chair' baada ya kupata ajali na kushindwa kufuatia kura alizopata kutotosha.
 

Inna Lillahi Wa Inna Ilaihi Rajjiuun!

No comments:

Post a Comment