Thursday, December 20, 2012

MAN UNITED YAKABIDHIWA REAL MADRID, ARSENAL v BAYERN MUNICH... BARCA YAPEWA AC MILAN 16-BORA KLABU BINGWA ULAYA... RONALDO ARUDI OLD TRAFFORD

Cristiano Ronaldo - Real Madrid


NYON, Uswisi
CRISTIANO Ronaldo atarejea Manchester United akiwa na mabingwa mara tisa Real Madrid katika mechi ya hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya huku Lionel Messi wa Barcelona akiwakabili AC Milan.

Bayern Munich, ambao msimu uliopita walifungwa katika fainali, watacheza dhidi ya Arsenal wakati Juventus itaikabili timu ambayo haikutarajiwa kufika hatua hiyo ya Celtic. Timu inayotumia pesa nyingi kusajili wachezaji ya Paris St Germain atacheza dhidi ya Valencia.

Lakini ratiba ya miamba wawili wa Hispania ndiyo iliyovutia tukio la leo katika makao makuu ya UEFA na wote wawili walipangiwa timu ambazo ni mabingwa wa zamani wa Ulaya.

Real, mabingwa wa Hispania, wamekuwa na msimu mbaya kwenye La Liga msimu huu na walimaliza wakiwa wa pili katika kundi lao la Ligi ya Klabu Bingwa nyuma ya Borussia Dortmund.

Lakini Ronaldo atakuwa na hamu kubwa ya kuiinua Real dhidi ya klabu yake ya zamani aliyoiongoza kutwaa ubingwa huo wa Ulaya mwaka 2008 na ambayo ilimsaidia kuwa mshambuliaji wa kiwango cha dunia.

Kocha wa Real, Jose Mourinho, ambaye aliwahi kuifundisha Chelsea, pia atakumbana na hasimu wake wa zamani Alex Ferguson.

"Ninaamini itakuwa mechi 'spesho' kwake (Ronaldo)," alisema Emilio Butragueno, mkurugenzi wa mahusiano wa Real Madrid. "Nadhani mashabiki watakuwa na furaha kubwa, kubwa sana kwa mechi hii itakayokuwa na mvuto wa aina yake.

"Itakuwa kitu kizuri kwa kila mmoja."

Barcelona hivi sasa wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa msimu huu lakini wamepangiwa timu yenye mafanikio makubwa zaidi yao katika michuano hiyo ya Ulaya AC Milan ambayo imetwaa ubingwa huo mara saba wakati michuano hiyo itakaporejea katikati ya Februari.

Messi amefunga magoli 90 mwaka 2012 na ameiongoza Barcelona kukaa kileleni mwa msimamo wa La Liga kwa tofauti ya pointi tisa wakati Milan wako pointi 14 nyuma ya vinara Juventus katika mbio za ubingwa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na walimaliza wa pili nyuma ya Malaga katika kundi lao.

Makamu wa rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu aliiambia televisheni ya Hispania ya Canal Plus: "Milan ni moja ya klabu kubwa za Ulaya na ni timu ambayo inaheshima kubwa.

"Hawafanyi vyema hivi sasa katika ligi yao lakini wana wachezaji wazuri. Hawako katika kiwango chao cha juu kwa sasa lakini soka hubadilika siku moja kwenda nyingine."

Katika mechi nyingine, Galatasaray watacheza dhidi ya Schalke 04, Shakhtar Donetsk watawakabili Dortmund na Porto watawavaa Malaga. 

   

Ratiba ya 16-Bora Ulaya

NYON, Ratiba ya Ligi ya 16-Bora Klabu Bingwa Ulaya iliyopangwa leo mjini Nyon, Uswisi: 

Galatasaray            v Schalke 04
Celtic                      v Juventus
Arsenal                   v Bayern Munich
Shakhtar Donetsk  v Borussia Dortmund
AC Milan               v Barcelona
Real Madrid           v Manchester United
Valencia                 v Paris St Germain
Porto                      v Malaga   
*Washindi wa pili wa hatua ya makundi wanaanzia nyumbani. 
* Mechi za kwanza zitachezwa Feb 12/13 na 19/20, za marudiano zitapigwa Machi 5/6 na 12/13

 

 Mechi za kwanza:
  
Feb. 12
    Celtic                     v Juventus
    Valencia                 v Paris St Germain  
  
Feb. 13
    Shakhtar Donetsk  v Borussia Dortmund
    Real Madrid           v Manchester United  
  
Feb. 19
    Porto                     v Malaga  
    Arsenal                  v Bayern Munich

  
Feb. 20 
    Galatasaray           v Schalke 04  
    AC Milan                v Barcelona  
  
    Marudiano
  
Machi 5
    Manchester United v Real Madrid
    Borussia Dortmund v Shakhtar Donetsk
  
Machi 6
    Paris St Germain    v Valencia
    Juventus                 v Celtic
  
Machi 12
    Schalke 04             v Galatasaray
    Barcelona               v AC Milan
  
Machi 13
    Malaga                   v Porto
    Bayern Munich       v Arsenal

1 comment:

  1. madrid hatoki kwa man u na barcelona anakufa kwa ac milan

    ReplyDelete